OR - TAMISEMI
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Afya), Dkt. Grace Magembe ametoa siku mbili kwa Mganga Mkuu wa hospitali ya Mtwara kuwasilisha taarifa ya ukaguzi wa dawa , vitendanishi pamoja na vifaa tiba katika Kituo cha Afya cha Ufukoni kilichopo katika Manispaa ya Mtwara Mikindani.
Agizo hilo limetolewa tarehe 26 Julai, baada ya Dkt. Magembe kutembelea kituo hicho na kubaini mapungufu katika leja za mapokezi na matumizi ya dawa , vifaa tiba na vitendanishi vya maabara.
Pia amemtaka kushirikiana na mkaguzi wa ndani wa Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani katika kutekeleza ukaguzi huo.
“ Haiwezekani dawa zitumike bila rekodi, TAMISEMI ilishatoa maelekezo na nyenzo ya ukaguzi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi, ni swala la utekelezaji tu,” amesema Dkt. Magembe
Pia amewaekekeza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mtwara na wa Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara kufanya mabadiliko ya uongozi katika Kituo cha Afya Ufukoni ikiwemo kumpangia majukumu mengine Mganga Mfawidhi wa kituo hicho.
Aidha, Dkt. Magembe ametumia fursa hiyo kuwahimiza Wakurugenzi wa Halmashauri za Mtwara na Nanyamba kuongeza kasi ya ujenzi unaoendelea katika Hospitali za Halmashauri.
Pia amewataka kuhakikisha wanatenga fedha za kumalizia kazi kwa haraka na ubora ili huduma zianze kutolewa.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment