Wakuu Wa Nchi Za Jumuiya Ya Madola Kukutana Rwanda


Na Mwandishi Maalum Kigali, Rwanda

MKUTANO wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Madola hatimaye unafanyika jijini Kigali, Rwanda baada ya kuahirishwa mara mbili (2020 na 2021) kwa sababu ya ugonjwa wa Corona.

Mkutano huo unaofanyika kuanzia tarehe 20 hadi 25 Juni 2022 umegawanywa katika makundi mbalimbali kama vile ya vijana, wanawake, wafanyabiashara, Mawaziri wa Mambo ya Nje, Wakuu wa Nchi pamoja na matukio ya pembezoni ambayo kwa pamoja mijadala yake inajikita katika maeneo matano.

Maeneo hayo ni utawala bora, utawala wa sheria, haki za binadamu; vijana, afya, teknolojia na uvumbuzi; maendeleo endelevu na mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.

Mkutano huo unaofanyika kwa kaulimbiu “Kufikia Mustakabali wa Pamoja: Kuunganisha, Kufanya uvumbuzi, Kufanya mabadiliko” (Delivering a Common Future: Connecting, Innovating, Transforming) umejipanga kujadili na kutafutia ufumbuzi wa changamoto zinazozikabili nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola ili kufikia maendeleo ya kweli katika nyanja zote.

Tanzania inashiriki kikamilifu katika mkutano huo na kimsingi masuala yanayojadiliwa yanakwenda sanjari na vipaumbele vya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Ikumbukwe, Rais Samia tangu aingie madarakani, Serikali yake imejipambanua katika kuheshimu haki za binadamu na kuzingatia masuala ya utawala wa sheria na demokrasia. Serikali ya awamu ya sita pia inafanya jitihada mbalimbali zenye lengo la kuyawezesha makundi maalum ya wanawake, vijana na wazee kiuchumi pamoja na kuhakikisha kuwa huduma za afya zinaboreshwa na zinapatikana kwa wananchi wote.

Aidha, mageuzi makubwa ya kiuchumi yameshuhudiwa katika Serikali ya awamu ya sita na uwekezaji mkubwa katika elimu na elimu ya ufundi unaendelea kufanyika` kwa lengo la kuchochea ubunifu bila kusahau mikakati madhubuti ya kukabiliana na madiliko ya tabianchi.



from MPEKUZI

Comments