Wachina Wapandishwa Kizimbani kwa Tuhuma za Uhujumu Uchumi


Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imewafikisha watuhumiwa wawili raia wa China katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mkoani Dar es Salaam, kwa makosa manne ikiwa ni pamoja na kukutwa na bidhaa ambazo hazijafuata taratibu za forodha, kukwepa kodi na uhujumu uchumi.

Washtakiwa hao Zhu Wei na Tao Pan wamefikishwa katika mahakama hiyo na kusomewa mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo Rita Tarimo.

Wakili wa serikali kutoka TRA Emmanuel Medalakini amaedai mahakamani hapo kuwa, watuhumiwa hao walikamatwa na mali hizo tarehe 13 mwezi huu katika eneo la Vingunguti mkoani Dar es Salaam ambapo wanadaiwa kushindwa kutoa nyaraka za kuthibitisha uhalali wa mali walizokutwa nazo.

Katika shtaka lingine, washtakiwa hao wanadaiwa kukwepa kulipa kodi ya zaidi ya shilingi milioni 400 huku wakijua kufanya hivyo ni kosa kisheria.

Baadhi ya bidhaa walizokamatwa nazo watuhumiwa hao ni vitenge, nyuzi za kushonea,vitambaa vya mapazia na mabegi ya Kompyuta mpakato vyote vikiwa vinatajwa kuingizwa nchini kwa njia ya magendo.

Washtakiwa hao hawakutakiwa kujibu chochote kutokana na mahakama ya Kisutu kutokuwa na mamlaka ya kusikiliza shauri hilo.

Wakili Medalikini pia ameieleza mahakama kuwa, upelelezi wa shauri hilo unaendela na uko mbioni kukamilika, hivyo washtakiwa hao wamerudishwa rumande hadi tarehe 29 mwezi huu kesi yao itakapotajwa tena.



from MPEKUZI

Comments