Uwekaji Vigingi Pori La Loliondo Hautoathiri Maendeleo Ya Wananchi-Majaliwa


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema zoezi la uwekaji wa vigingi katika eneo la kilometa za mraba 1,500 la Pori Tengefu la Poloreti-Loliondo ambalo limekamilika kwa asilimia 100 halitoathiri maendeleo ya wakazi waishio kwenye eneo la vijiji 14 vinavyopakana na eneo hilo.

Hata hivyo, Mheshimiwa Majaliwa amesisitiza kwamba hakutakuwepo na kijiji chochote kitakachofutwa na hakuna miundombinu itakayoondolewa kwa kuwa ndani ya eneo la kilometa za mraba 1,500 hakuna miundombinu yoyote.

Ameyasema hayo jana(Alhamisi, Juni 30, 2022) wakati akitoa Hoja ya Kuahirisha Mkutano wa Saba wa Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bungeni jijini Dodoma. Amesema    Serikali imesimamia kwa umakini mkubwa zoezi la uwekaji vigingi kwenye hilo ambalo ni muhimu kwa ikolojia ya Hifadhi ya Serengeti na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.

Mheshimiwa Masema Serikali imeendelea kushirikiana na wananchi wa Loliondo katika kuboresha malisho ya mifugo, uchimbaji wa visima vya maji, ujenzi wa majosho pamoja na miundombinu ya kunyweshea mifugo kwenye eneo la kilometa za mraba 2,500. 

“Pia, ninaielekeza Wizara ya Maliasili na Utalii kushirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na wadau wengine kuhakikisha kuwa Sheria ya Ardhi ya vijiji namba 5 ya mwaka 1999 inatumika ipasavyo kutenga na kuweka mipaka ya vijiji.”

Amesema  Serikali kwa kuzingatia matakwa ya wananchi hasa maeneo ya malisho kwenye vijiji 14 vilivyopo karibu na Pori Tengefu la Poloreti itaweka utaratibu utakaopangwa kwa pamoja baada ya kukamilisha zoezi la utambuzi wa mifugo kwenye vijiji husika.

Mheshimiwa Majaliwa amesema katika kuhakikisha uwepo wa matumizi endelevu ya Pori Tengefu la Poloreti, Serikali ilielekeza eneo la kilometa za mraba 1,500 lihifadhiwe na eneo lililobaki la kilometa za mrada 2,500 wananchi waendelee kulitumia kwa shughuli nyingine.

Akizungumzia kuhusu zoezi la wakazi wa Ngorongoro kuhama kwa hiari katika eneo kwa ajili ya kupisha uhifadhi endelevu, Waziri Mkuu amesema kumekuwa na mafanikio makubwa katika kusimamia utekelezaji wa zoezi hilo hadi kufikia tarehe 09 Juni 2022, jumla ya kaya 293 zenye watu 1,497 zimejiandikisha. “Serikali imeendelea kuhamasisha na kuandikisha zile kaya ambazo zipo tayari kuhama kwa hiari.”

“Upendo huo uliooneshwa na Mheshimiwa Samia, Rais wetu hauna budi kupongezwa na kila mwenye kuitakia mema nchi hii. Hata hivyo, utaratibu huu ni maalum kwa Ngorongoro pekee. Leo tarehe 30 Juni, 2022 kaya nyingine 25 zenye jumla ya watu 115 zinatarajiwa kusafiri kwa hiari kuelekea Msomera na kuendelea na maisha yao kama kawaida.” 

Wakati huo huo, Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii isianze zoezi upandishwaji hadhi wa maeneo ya mapori tengefu kuwa mapori ya akiba hilo hadi wananchi watoe maoni yao kwa maslahi ya pande zote.

“Niwahakikishie wananchi wa maeneo husika kwamba utaratibu wa kupandisha hadhi maeneo ya mapori hayo kuwa mapori ya akiba utasubiri mapitio ya pamoja kati ya Serikali na wananchi. Tathmini hiyo na ushirikishwaji wa wananchi husaidia Serikali kufanya maamuzi ya iwapo kuendelea na utaratibu wa kupandisha hadhi au la Hivyo, Wizara isianze zoezi hilo hadi wananchi watoe maoni yao kwa maslahi ya pande zote.”

Amesema rasilimali za wanyamapori ni muhimu kwa maendeleo ya nchi, hususan katika kukuza utalii na hivyo kuongeza pato la Taifa. “Kwa msingi huo, mpango wa Serikali kupandisha hadhi baadhi ya mapori tengefu kuwa mapori ya akiba ni katika kuimarisha ulinzi wa rasilimali zilizopo katika mapori hayo kwa uhifadhi endelevu.” 

Hata hivyo,  Waziri Mkuu amesema utaratibu wa kutangazwa kwa eneo  lolote kuwa Pori la Akiba hufanywa na Mheshimiwa Rais kwa kufuata taratibu zilizowekwa kisheria ikiwemo kufanya tathmini ya kina ya umuhimu wa eneo husika katika uhifadhi na ushirikishwaji wa wananchi kupitia Mamlaka za Serikali za Mitaa za maeneo husika.




from MPEKUZI

Comments