Na. Farida Ramadhani na Peter Haule, WFM, Dodoma
Serikali imezielekeza Taasisi zote nchini kuzingatia matakwa ya Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2013 na umuhimu wake katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Hayo yameelezwa bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Hamad Hassan Chande, alipojibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Eng. Mwanaisha Ng'azi Ulenge, aliyetakakujua wakati ambao Serikali itafanya tathmini kuhusu utekelezaji wa Sheria ya Manunuzi wa Umma ya Mwaka 2013 katika Sehemu ya 64(2)(C) ya Kanuni ya 30 C kama ilivyofanyiwa Marekebisho.
Mhe. Chande alisema katika kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Ununuzi wa Umma, SURA 410 pamoja na kanuni zake, Mamlaka ya Kudhibiti Ununuzi wa Umma (PPRA) hufanya tathmini ya ununuzi na kuchapisha taarifa ya tathmini hiyo kila mwaka.
“Matokeo ya tathmini ya mwaka 2020/21 kuhusu kutenga fedha za ununuzi asilimia 30 kwa makundi maalumu imeonesha kuwa, kati ya taasisi 86 zilizofanyiwa ukaguzi, taasisi mbili (2) zilitenga fedha hizo, taasisi tatu (3) zilitenga kiwango pungufu na taasisi 81 hazikutenga kabisa”, alibainisha Mhe. Chande.
Aidha, aliviagiza Vitengo vya Ukaguzi wa Ndani kuhakikisha kuwa Ripoti za kila Robo Mwaka ambazo huwasilishwa PPRA kuwa na taarifa kuhusu utekelezaji wa sheria katika eneo hilo.
Wakati huohuo, Mhe. Chande alisema katika mwaka 2021/22 Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inakamilisha tathmini ambayo itabainisha maeneo yenye uhitaji wa kujengwa ofisi za Mamlaka hiyo nchini kulingana na vigezo vilivyowekwa.
Alisema Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inautaratibu wa kupitia na kufanya tathmini kwa nchi nzima yenye lengo la kubaini maeneo yote yenye uhitaji wa kujengwa ofisi za TRA kwa ajili ya ufuatiliaji, usimamizi na ukusanyaji kodi ili kusogeza huduma za kikodi karibu na wananchi.
“Utaratibu huu unazingatia pamoja na mambo mengine, uwiano wa gharama za ukusanyaji wa mapato na kiwango cha kodi kinachotarajiwa kukusanywa wakati ofisi hizo zitakapofunguliwa kutokana na shughuli mbalimbali za kiuchumi katika eneo husika”, alifafanua Mhe. Chande.
Alisema Serikali inadhamiria kuhakikisha kuwa maeneo yote ikiwemo Wilaya ya Mkalama yatakayokidhi vigezo stahiki yanajengwa ofisi za TRA
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment