Serikali Yawasilisha Muswada Wa Sheria Ya Fedha Wa Mwaka 2022 Bungeni

  1. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba Muswada wa Sheria ya Fedha ya Mwaka 2022 (The Finance Act, 2022) pamoja na marekebisho yake sasa usomwe kwa mara ya pili.

  1. Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa Kamati ya Bunge ya Bajeti chini ya Mwenyekiti wake Mheshimiwa Sillo Daniel Baran, Mbunge wa Babati Vijijini kwa kuujadili kwa kina Muswada huu na kutoa ushauri mbalimbali ili kuuboresha.

  1. Mheshimiwa Spika, napenda kulihakikishia Bunge lako tukufu kwamba, Muswada huu umezingatia kwa kiasi kikubwa ushauri na mapendekezo ya wadau mbalimbali hususan Kamati ya Bunge ya Bajeti na Waheshimiwa Wabunge wengine wote wakati wakichangia katika hotuba ya bajeti ya Serikali iliyopitishwa hapa Bungeni tarehe 24 Juni, 2022. Aidha, namshukuru pia Mwanasheria Mkuu wa Serikali, waandishi wa Sheria, wataalam wa Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kuandaa Muswada huu pamoja na marekebisho yake. Vilevile, natoa shukrani za dhati kwa Waziri wa Fedha wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mheshimiwa Saada Mkuya, Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar pamoja na wataalam wake kwa mashauriano tuliyofanya ili kuhakikisha kwamba Sheria za kodi tunazozitekeleza baina ya pande mbili za Muungano hazileti mgongango katika utekelezaji.

  1. Mheshimiwa Spika, lengo la Muswada huu ni kutekeleza kisheria, hatua za mapato zinazohusu Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2022/2023 niliyoiwasilisha Bungeni tarehe 14 Juni mwaka huu. Muswada huu unafanyia marekebisho ya sheria thelathini na Tano zinazohusu masuala ya fedha, kodi, ushuru na tozo kwa lengo la kuweka, kurekebisha, kupunguza au kufuta viwango vya kodi, ushuru, ada na tozo. Lengo la kurekebisha Sheria hizi ni kuweka mfumo wa kodi ambao ni tulivu na unaotabirika, kuboresha taratibu za ulipaji na ukusanyaji kodi na kuweka na kuboresha mazingira ya kufanya biashara na uwekezaji ili kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi na kuongeza mapato ya Serikali.

  1. Mheshimiwa Spika, kufuatia marekebisho yaliyofanyika kupitia Jedwali la Marekebisho, Sheria zinazofanyiwa marekebisho ni zifuatazo:-
  2. i)Sheria ya Magonjwa ya Wanyama, Sura ya 156;
  3. ii)Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania, Sura ya 197;

iii)       Sheria ya Usajili wa Majina ya Biashara, Sura ya 213;

  1. iv)Sheria ya Korosho, Sura ya 203;
  2. v)Sheria ya Usajili wa Makampuni, Sura ya 212;
  3. vi)Sheria ya Hakimiiliki, Sura ya 218;

vii)      Sheria ya Tasnia ya Maziwa, Sura ya 262;

viii)    Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, Sura ya 147;

  1. ix)Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta, Sura ya 306
  2. x)Sheria ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji, Sura ya 414;
  3. xi)Sheria ya Usafirishaji Bidhaa Nje ya Nchi, Sura ya 196;

xii)      Sheria ya Mbolea, Sura ya 378;

xiii)    Sheria ya Magari ya Kigeni, Sura ya 84;

xiv)    Sheria ya Michezo ya Kubahatisha, Sura ya 41;

  1. xv)Sheria ya Mikopo ya Serikali, Dhamana na Misaada, Sura ya 134;

xvi)    Sheria ya Ngozi na Bidhaa za Ngozi, Sura ya 120;

xvii)   Sheria ya Kodi ya Mapato, Sura 332;

xviii)  Sheria ya Bima, Sura ya 394;

xix)    Sheria ya Ardhi, Sura ya 113;

  1. xx)Sheria ya Udhibiti wa Usafirishaji wa Nchi Kavu, Sura ya 413;

xxi)     Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa, Sura ya 290;

xxii)   Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya), Sura ya 287;

xxiii) Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji), Sura ya 288;

xxiv) Sheria ya Madini, Sura ya 123;

xxv)   Sheria ya Mifumo ya Malipo, Sura ya 437;

xxvi) Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi, Sura ya 297;

xxvii)    Sheria ya Bandari, Sura ya 166;

xxviii)   Sheria ya Uwekezaji, Sura ya 38;

xxix) Sheria ya Mamlaka ya Mapato Tanzania, Sura ya 399;

xxx)   Sheria ya Wakala wa Meli, Sura ya 415;

xxxi)   Sheria ya Usimamizi wa Kodi, Sura 438;

xxxii)    Sheria ya Rufani za Kodi, Sura ya 408;

xxxiii)   Sheria ya Usajili wa Wadhamini, Sura ya 318;

xxxiv)   Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, Sura ya 148; na

xxxv)    Sheria ya Mafunzo na Ufundi Stadi, Sura ya 82;

  1. Mheshimiwa Spika, kufuatia majadiliano na wadau mbalimbali hususan michango ya Wabunge wakati wakijadili bajeti ya Serikali kwa mwaka 2022/23 na maoni ya Kamati ya Bunge ya Bajeti, Serikali imefanya marekebisho mbalimbali ya hatua za mapato zilizowasilishwa kupitia hotuba ya bajeti ikiwemo yafuatayo; 

(i)         kupunguza kiwango cha kodi kwenye zawadi ya ushindi (Gaming Tax on Winnings) kutoka asilimia 15 hadi asilimia 10 kwenye michezo ya kubahatisha ya ubashiri wa matokeo ya michezo (Sports betting). Lengo la hatua hii ni kuongeza mapato ya Serikali kutokana na watu wengi zaidi kuhamasika kushiriki kwenye michezo ya kubahatisha ya kubashiri matokeo ya michezo. Uchambuzi uliofanyika umebainisha kwamba endapo Serikali itaendelea kupunguza kiwango husika hadi kufikia asilimia 10 mapato ya Serikali yataongezeka kutoka shilingi bilioni 4.2 hadi kiasi cha shilingi bilioni 5.2 kutokana na watu wengi zaidi kuhamasika kushiriki katika michezo hiyo; 

(ii)       kutofanya marekebisho ya kubadili mgawanyo wa asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri ili kuhudumia miundombinu ya masoko ya machinga. Serikali itatumia fedha zilizotengwa kwa ajili ya kutoa mikopo kwa wajasiriamali katika bajeti ya mwaka 2022/23 (bilioni 1 kwa kila Mkoa) kwa Halmashauri za Majiji na Manispaa zitumike kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu na masoko ya machinga; 

(iii)      kuondoa pendekezo la kutoza Kodi ya Zuio kwa kiwango cha asilimia 2 kwenye malipo ya wachimbaji wadogo wa madini (Small Scale Miners). Utozaji wa kodi husika utasababisha utoroshaji wa madini na kupunguza kasi ya wachimbaji kuuza madini husika katika masoko ya madini (Buying Centres/Gem Houses) au vituo vya uchenjuaji (refinery centres);

(iv)      kuondoa hatua ya kutoza kodi ya awali ya mapato (advance income tax) ya shilingi 20 kwa lita kwa wafanyabiashara wa rejareja wa mafuta ya petroli nchini ambayo ingekusanywa na waingizaji wa mafuta hayo kwa jumla na kulipwa Serikalini. Hatua hii inatokana na kutotabirika kwa bei za mafuta ambazo zilionekana kuanza kushuka mwezi Mei, 2022 lakini bei hizo sasa zinaonekana kupanda;

(v)       kufanya maboresho kwenye Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye mafuta ya kula yanayozalishwa nchini kwa kutumia mbegu zinazozalishwa nchini sambamba na kusamehe kodi hiyo kwenye malighafi na vifungashio vinavyotumika katika uzalishaji. Lengo la hatua hii ni kuleta unafuu wa bei ya mafuta ya kula iliyopanda kutokana na mdororo wa uchumi na kulinda misingi ya Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani inayoelekeza bidhaa zinazouzwa ndani ya nchi zisamehewe kodi hiyo (exempted) badala ya kutozwa kodi ya asilimia 0 (zero rated) ili kurahisisha utekelezaji wa msamaha huu;

(vi)      Serikali imefanya uamuzi wa kubadilisha mfumo wa uendeshaji wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) ili taasisi hiyo isijihusishe na jukumu la uwakala wa forodha na badala yake ibaki na jukumu la kusimamia na kudhibiti watoa huduma za usafiri majini. Hata hivyo, taasisi hii itaendelea na shughuli za uwakala wa forodha kwenye bidhaa za makinikia, silaha na vilipuzi, nyara za Serikali na wanyama hai wanaotambulika kwa mujibu wa Sheria ya Wanyamapori. Hatua hii itaondoa mgongano wa kimaslahi unaotokana na TASAC kuwa mtoa huduma za uwakala wa forodha na mdhibiti wa watoa huduma za usafiri majini kwa wakati mmoja;

(vii)    kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Ardhi, Sura 113 ili kuweka utaratibu kwa Waziri mwenye dhamana ya masuala ya Fedha baada ya kufanya mashauriano na Waziri mwenye dhamana ya masuala ya Ardhi mamlaka ya kusamehe riba ya malimbikizo ya pango la ardhi. Lengo la hatua hii ni kuhamasisha ulipaji kodi kwa hiari na kuongeza mapato ya serikali kwa kukusanya malimbikizo ya kodi husika; na

(viii)   kuongeza wigo wa kusamehe tozo ya mafunzo ya ufundi stadi kwa wahitimu wa elimu ya juu na vyuo vya kati badala ya vyuo vikuu pekee kama nilivyopendekeza awali kwenye Hotuba ya Bajeti. Lengo la hatua hii ni kuongeza idadi ya wanufaika wa mafunzo ya vitendo ya kuwapatia ujuzi na uzoefu wa kazi kabla ya ajira kupitia Wakala wa Huduma za Ajira Tanzania (TAESA).

(ix)      Kusogeza muda wa kufutwa kwa msamaha wa kodi ya Ongezeko la thamani kwenye huduma za kukodi ndege (air charter service) kwa kipindi cha miezi 6 kuanzia tarehe 1 Julai, 2022 ili kutoa fursa ya utekelezaji wa miadi iliyowekwa kwa kuzingatia uwepo wa msamaha huo.

  1. Mheshimiwa Spika, Aidha, ili kuboresha taratibu za usimamizi na ukusanyaji wa kodi ya mapato kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na upande wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, na kufuatia mashauriano na Waziri mwenye dhamana na masuala ya fedha wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, tumefanya marekebisho ya Sheria ya Kodi ya Mapato na Sheria ya Usimamizi wa Kodi ili kuwezesha yafuatayo;

                     (i)         kumwezesha Waziri mwenye dhamana na masuala ya Fedha wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya mashauriano na Waziri mwenye dhamana na masuala ya fedha wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kuweka viwango mfuto  vya kodi kwa walipa kodi binafsi wadogo (presumptive rates) vitakavyotumika Tanzania Zanzibar;

                    (ii)         kutoa nafuu ya kodi ya mapato kwa kuwezesha kampuni zinazofanya biashara pande mbili za Muungano kupata nafuu ya kodi inayolingana na kodi iliyolipwa upande wowote wa Muungano ili kuepusha utozaji kodi mara mbili; Katika kutekeleza hatua hii, Sheria ya Usimamizi wa Kodi, Sura 438 itatambua namba ya utambulisho ya mlipakodi aliyesajiliwa Tanzania Zanzibar ili kurahisisha taratibu za ukusanyaji kodi kwa kampuni zenye ofisi pande mbili za Muungano;

         Pamoja na marekebisho hayo ya Sheria, Mamlaka ya Mapato Tanzania na Bodi ya Mapato ya Tanzania Zanzibar zitasaini Hati ya Makubaliano ili kuwezesha utekelezaji wa Sheria hizi.

MAUDHUI YA MUSWADA: 

  1. Mheshimiwa Spika, Muswada huu umegawanyika katika sehemu Thelathini na Sita kama ifuatavyo: –
  2. Mheshimiwa Spika, Sehemu ya Kwanza, inahusu masuala ya utangulizi inayojumuisha jina na tarehe ya kuanza kutumika kwa Sheria hii ambapo Sheria itaanza kutumika tarehe 1, Julai 2022.
  3. Mheshimiwa Spika, Sehemu ya Pili, Nane, Kumi na Moja, Kumi na Tatu, Ishirini na moja, na Thelathini na Mbili kama zilivyorekebishwa, zinapendekeza kurekebisha Sheria ya Magonjwa ya Wanyama, Sura ya 156; Sheria ya Tasnia ya Maziwa, Sura ya 262; Sheria ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji, Sura ya 414, Sheria ya Mbolea, Sura ya 378; Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu, Sura ya 413; na Sheria ya Wakala wa Meli Tanzania, Sura ya 415, ili kuondoa mwingiliano wa sheria mbalimbali za taasisi za udhibiti hususan kwa kurejesha suala la usimamizi wa viwango kusimamiwa na Shirika la Viwango Tanzania badala ya utaratibu wa sasa ambapo kila Taasisi ya udhibiti ina mamlaka ya kusimamia masuala ya viwango kwenye eneo lake. Lengo la marekebisho haya ni kuhakikisha shughuli za udhibiti wa viwango zinafanywa na Taasisi moja ili kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji. Hata hivyo, kupitia Jedwali la marekebisho, mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania Sura ya 172, yameondolewa kwenye Muswada huu kutokana na unyeti wa shughuli za mawasiliano. 
  1. Mheshimiwa Spika, Sehemu ya Tatu kama ilivyorekebishwa, inapendekeza kufanya marekebisho katika Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania, Sura ya 197  kwenye vifungu vya 35(2) na 36(1) ili kuongeza kiwango cha ukomo wa Serikali kukopa kutoka Benki Kuu. Lengo la marekebisho haya ni kuiwezesha Serikali kutekeleza Bajeti zake kwa ufanisi hususan kwenye kutekeleza miradi ya maendeleo.  
  2. Mheshimiwa Spika, Sehemu ya Nne kama ilivyorekebishwa inapendekeza marekebisho katika Sheria ya Usajili wa Majina ya Biashara, Sura ya 213 ili:

(i)         kuongeza tafsiri ya neno “beneficial owner” ili kuwianisha tafsiri hiyo na ile iliyotolewa katika Sheria ya Kudhibiti Utakasishaji wa Fedha Haramu, Sura ya 423;

(ii)       kuweka sharti la kuwasilisha taarifa za wamiliki wanufaika wakati wa usajili wa biashara zinazoendeshwa kwa ubia;

(iii)      kubainisha watu au taasisi ambazo zinaweza kupata taarifa za mmiliki mnufaika; na

(iv)      kuweka faini kwa kushindwa kutoa taarifa zinazohusiana na wamiliki wanufaika wa ubia.

Lengo la marekebisho haya ni kuhakikisha uzingatiaji wa sheria na upatikanaji wa taarifa za wamiliki wanufaika.

  1. Mheshimiwa Spika, Sehemu ya Tano inapendekeza marekebisho kwenye kifungu cha 17A cha Sheria ya Korosho, Sura ya 18 ili kuainisha mgawanyo wa mapato yatokanayo na korosho ambapo asilimia 50 itaenda Mfuko Mkuu wa Hazina, na asilimia 50 itagawanywa kwenye Mfuko wa Maendeleo ya Kilimo na ruzuku za pembejeo za kilimo. Lengo la marekebisho haya ni kuwezesha maendeleo ya sekta ya kilimo kwa kusaidia upatikanaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya ruzuku, pembejeo na maendeleo ya kilimo.

  1. Mheshimiwa Spika, Sehemu ya Sita kama ilivyorekebishwa inapendekeza marekebisho ya Sheria ya Makampuni, Sura ya 212 kama ifuatavyo;

(i)         Kama ilivyofanyika kwenye marekebisho ya Sheria ya Usajili wa Majina ya Biashara, Sura ya 213, kuongeza tafsiri ya neno “beneficial owner” ili kuwianisha tafsiri hiyo na ile iliyotolewa katika Sheria ya Kudhibiti Utakasishaji wa Fedha Haramu, Sura ya 423;

(ii)       kuweka adhabu kwa makampuni ambayo yatashindwa kutunza rejesta ya wanachama na wamiliki wanufaika au kutoa taarifa ya mabadiliko kwenye rejesta, kushindwa kuweka fahirisi ya majina ya wanachama na wamiliki wanufaika wa kampuni na kushindwa kuwasilisha ritani ya kila mwaka ya kampuni;

(iii)      kuweka adhabu kwa makampuni ambayo yatashindwa kutunza rejesta ya wanachama na wamiliki wanufaika au kutoa taarifa ya mabadiliko kwenye rejesta, na kushindwa kuweka fahirisi ya majina ya wanachama na wamiliki wanufaika wa kampuni; na

(iv)      kuweka wajibu kwa wafilisi wa makampuni kutunza kumbukumbu za hesabu na nyaraka zinazohusiana na ufilisi wa Makampuni.

  1. Mheshimiwa Spika, Sehemu ya Saba kama ilivyorekebishwa inapendekeza marekebisho ya Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki, Sura ya 218 ili;

(i)         kuongeza tafsiri ya maneno “collective management” na “collective management organization” ili kuwezesha ufanisi kwenye utekelezaji wa Sheria;

(ii)       ili kuondoa mgongano wa kimaslahi katika kutekeleza majukumu ya Chama cha Hakimiliki Tanzania na Ofisi ya Hakimiliki;

(iii)      kutenganisha majukumu ya Ofisi ya Hakimiliki na majukumu ya taasisi za usimamizi jumuishi na kuainisha majukumu ya Ofisi hiyo;

(iv)      kuanzisha tozo ya asilimia 1.5 kwenye vifaa vinavyotumika kuzalisha, kusambaza, kurudufu na kutunza kazi za sanaa ambavyo ni radio/tv set enabling recording, analogue audio recorders, analogue video recorders, CD/DVD copier, digital jukebox and mp3 player; vinavyotumika kuwezesha kuzalisha, kusambaza, kurudufu na kutunza kazi za sanaa, uandishi na ubunifu mwingine; na

(v)       kubainisha majukumu ya Ofisi ya Hakimiliki na kuweka mfumo wa usimamizi jumuishi wa hakimiliki na kuweka wajibu kwa taasisi za usimamizi jumuishi kuwasilisha Ofisi ya Hakimiliki taarifa zao za utendaji na hesabu zilizokaguliwa.

Lengo la marekebisho haya ni kuongeza uwajibikaji na kuimarisha usimamizi wa masuala yanayohusu hakimiliki na hakishirikishi.

  1. Mheshimiwa Spika, Sehemu ya Tisa kama ilivyorekebishwa, inapendekeza marekebisho katika Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, Sura ya 147 kama ifuatavyo;

(i)         kuwianisha mfumo wa adhabu katika sheria za kodi ili kuhakikisha kuwa adhabu zitakazotumika dhidi ya makosa ya kikodi ni zile zilizoainishwa katika Sheria ya Usimamizi wa Kodi, Sura ya 438;

(ii)       kujumuisha katika sheria watoa huduma wa televisheni za kulipia wanaotumia miundombinu mingine tofauti na ile ya ardhini;

(iii)      kurekebisha Jedwali la Nne ili kubainisha viwango vya ushuru wa bidhaa kwenye bidhaa za sukari na betri za maji kwa lengo la kupanua wigo wa kodi na kulinda afya za walaji na mazingira. Aidha, kupitia marekebisho yaliyofanyika kwenye kupitia Jedwali la Marekebisho, bidhaa za sukari zinazoagizwa kutoka nje ya nchi zitatozwa ushuru wa bidhaa kwa kiasi cha shilingi 1,000 na bidhaa za aina hiyo zinazozalishwa nchini hazitatozwa. Aidha, betri kutoka nje ya nchi zitatozwa ushuru wa asilimia 10 na bidhaa za aina hiyo zinazozalishwa nchini zitatozwa asilimia 5. Vilevile, Jedwali linarekebishwa ili kusamehe ushuru wa bidhaa kwenye vifungashio vya maua, matunda na mbogamboga kwa lengo la kuwapunguzia gharama wauzaji wa bidhaa hizo nje ya nchi na kuongeza ushindani wa bidhaa hizo katika masoko ya kimataifa.

  1. Mheshimiwa Spika Sehemu ya Kumi kama ilivyorebishwa inapendekeza marekebisho ya Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta, Sura ya 306 kwa kuongeza kifungu kipya cha 164B ili kutoza ada ya matumizi ya kisimbuzi kuanzia shilingi 500 hadi 2,000 kulingana na kiwango cha matumizi kwa lengo la kuongeza mapato ya Serikali. Mchanganuo wa utozaji wa ada hii kulingana na matumizi utabainishwa kwenye Kanuni.

  1. Mheshimiwa Spika, Sehemu ya Kumi na Mbili inapendekeza marekebisho ya Sheria ya Usafirishaji Bidhaa Nje ya Nchi, Sura ya 196 ambapo Jedwali linarekebishwa ili kuweka tozo ya usafirishaji wa shaba chakavu na vyuma chakavu nje ya nchi. Lengo la marekebisho haya ni kulinda viwanda vya ndani na kuhakikisha upatikanaji wa malighafi kwa viwanda vya ndani vya bidhaa za shaba na chuma.

  1. Mheshimiwa Spika Sehemu ya Kumi na Nne inapendekeza marekebisho ya Sheria ya Magari ya Kigeni, Sura ya 84 kwa kupunguza ada ya magari ya kigeni yanayozidi ekseli 3 yanayopita nchini kwa lengo la kuwianisha viwango vya ada zinazotozwa nchini na zile zinazotozwa katika ukanda wa Jumuiya ya Afrika Masharika, Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika, na Soko la Pamoja la Mashariki na Kusini mwa Afrika.

  1. Mheshimiwa Spika, Sehemu ya Kumi na Tano kama ilivyorekebishwa inapendekeza marekebisho ya Sheria ya Michezo ya Kubahatisha, Sura ya 41 kama ifuatavyo:

(i)         kupunguza kiwango cha kodi kinachohusiana na zawadi ya ushindi kutoka asilimia 15 hadi 10 kwenye michezo ya kubashiri matokeo;

(ii)       kuainisha masharti ya Sheria ya Usimamizi wa Kodi,Sura 438 yatakayotumika katika kodi ya michezo ya kubahatisha; na

(iii)      kuweka utaratibu wa ukusanyaji wa kodi kwenye zawadi za ushindi katika michezo ya kubahatisha.

  1. Mheshimiwa Spika, Sehemu ya Kumi na Sita inapendekeza marekebisho ya Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada ya Serikali, Sura ya 134 ili kuongeza ufanisi katika usimamizi wa deni la taifa kwa kufanya yafuatayo:

(i)   kuboresha utaratibu wa ukokotoaji wa uhimilivu wa deni kwa kutumia uchambuzi wa madeni unaotumia kipimo zaidi ya kimoja;

(ii)  kumwezesha Kamishna wa Usimamizi wa Madeni kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Wataalam na kuboresha uwakilishi wa wajumbe katika Kamati ya Wataalamu; na

(iii)  kuipa jukumu Idara ya Usimamizi wa Madeni la kufanya kazi ya uchambuzi na uandaaji wa nyaraka zinazowasilishwa kwenye Kamati za Madeni.

  1. Mheshimiwa Spika, Sehemu ya Kumi na Saba inapendekeza marekebisho ya Sheria ya Ngozi na Bidhaa za Ngozi, Sura ya 120 ili kuondoa ngozi au bidhaa za ngozi za wanyamapori katika wigo wa Sheria hiyo. Lengo la marekebisho haya ni kuondoa mgongano wa sheria na mwingiliano wa majukumu kati ya vyombo vinavyosimamia ngozi na bidhaa za ngozi za wanyama wa majumbani na vile vinavyosimamia ngozi na bidhaa za ngozi za wanyamapori.

  1. Mheshimiwa Spika, Sehemu ya Kumi na Nane kama ilivyorekebiswa inapendekeza marekebisho ya Sheria ya Kodi ya Mapato, Sura ya 332 kama ifuatavyo:

(i)         kuongeza tafsiri ya maneno “digital market place,” “electronic services”  ili kuwezesha utozaji kodi kwenye huduma za kidigitali;

(ii)       kuongeza tafsiri ya maneno “alternative financing arrangement” na kurekebisha kifungu cha 32 ili kuwianisha maana ya riba inayotolewa kwa mikopo ya kawaida ya kibenki kuwa sawa na faida kwa mikopo mbadala;

(iii)      kuweka utaratibu maalum wa kulipa kodi kwa wamiliki wa mabasi na malori kwa viwango maalumu kulingana na ukubwa wa gari;

(iv)      kuondoa kwenye wigo wa kutozwa kodi faida ambayo haijagawanywa na taasisi za fedha za ndani ya nchi zilizo na matawi nje ya nchi kwa misingi au taratibu zilizowekwa na Benki Kuu ya Tanzania;

(v)       kumpa Waziri mamlaka ya kusamehe kodi ya mapato kwa wawekezaji mahiri maalumu baada ya kupata ridhaa ya Baraza la Mawaziri. Lengo la marekebisho haya ni kuwianisha masharti ya Sheria hii na masharti ya Sheria ya Uwekezaji kuhusu utaratibu wa kutoa misamaha ya kodi;

(vi)      kujumuisha uendeshaji na usimamizi wa biashara unaofanyika kwa njia za kielektroniki;

(vii)    kuongeza malipo ya utumiaji rasilimali pamoja na huduma za kidigitali zinazotolewa na watoa huduma wasio wakaazi hapa nchini kwa lengo la kupanua wigo wa kodi;

(viii)   kuwezesha wapangaji binafsi kuzuia kodi ya mapato kwenye malipo ya pango ya nyumba za biashara na makazi; Pia Sheria inarekebishwa ili kuondoa sharti la kukata kodi ya zuio kwenye malipo ya pango ya nyumba za biashara na makazi. Lengo la marekebisho haya ni kuleta ufanisi wa ukusanyaji wa kodi ya pango na kuongeza vyanzo mbadala vya fedha kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo;

(ix)      kutoza kodi ya mapato ya asilimia 2 kwenye malipo yanayofanywa kwa watoa huduma za kidijitali wasio wakaazi kwa lengo la kupanua wigo wa kodi na kuongeza mapato ya Serikali;

(x)       ili kuwaondolea wajibu wa kuwasilisha ritani za kodi ya mapato walipakodi wa kidijitali wasio wakaazi;

(xi)      kumwezesha Waziri mwenye dhamana na masuala ya Fedha wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya Mashauriano na Waziri mwenye dhamana na masuala ya fedha wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kuweka viwango mfuto vya kodi kwa walipa kodi binafsi wadogo vitakavyotumika Tanzania Zanzibar;

(xii)    kutoa nafuu ya kodi ya mapato kwa kuwezesha kampuni zinazofanya biashara pande mbili za Muungano kupata nafuu ya kodi inayolingana na kodi iliyolipwa upande wowote wa Muungano ili kuepusha utozaji kodi mara mbili; Katika kutekeleza hatua hii, Sheria ya Usimamizi wa Kodi, Sura 438 itatambua namba ya utambulisho ya mlipakodi aliyesajiliwa Tanzania Zanzibar ili kurahisisha taratibu za ukusanyaji kodi kwa kampuni zenye ofisi pande mbili za Muungano;

(xiii)   kurekebisha Jedwali la Kwanza ili kurekebisha kiwango cha kodi kwenye daraja la juu la mauzo kwa walipakodi binafsi wadogo ili kuongeza uwazi na kurahisisha ukadiriaji na ulipaji wa kodi. Aidha, Jedwali la Kwanza linarekebishwa kwa kupunguza kiwango cha kodi ya zuio kwa malipo ya mrabaha ya filamu kwa watoa huduma wa nje na ndani ya nchi kwa lengo la kuongeza ajira, kukuza tasnia ya filamu na kuchochea uhaulishaji wa ujuzi; na

(xiv)   kurekebisha Jedwali la Pili ili kusamehe kodi ya ongezeko la mtaji kwenye uhamishaji wa haki na taarifa za uchimbaji madini kwenda Kampuni za Ubia, uhamishaji wa hisa kwenda Serikalini, na kwenye hisa ambazo Serikali imepata kupitia Msajili wa Hazina. Lengo la marekebisho haya ni kuwezesha Serikali kutekeleza majukumu yake ya kimkataba na kuhakikisha kuwa uhamishaji wa haki na taarifa za madini unafanyika kwa wakati.

Aidha, kama nilivyoeleza awali, kupitia Jedwali la marekebisho, Serikali imeondoa pendekezo la kutoza kodi ya zuio kwa wachimbaji wadogo wa madini na kuondoa sharti kwa waagizaji wa nishati ya mafuta kwa jumla kuwa mawakala wa ukusanyaji kodi wa Serikali kutoka kwa wauzaji wa reja reja



from MPEKUZI

Comments