Serikali Kuhakikisha Huduma Za Vipimo Vya Sikoseli Zinapatikana Katika Vituo Vya Afya Nchini


NA WAF-ARUSHA

Serikali kupitia Wizara ya Afya imeingiza ugonjwa wa Sikoseli katika mpango mkakati wa kupambana na magonjwa yasiyoambukiza ili kuweza kupambana nao na kuhakikisha huduma za vipimo na matibabu zinapatikana katika vituo vya kutolea huduma za afya ngazi ya msingi.

Hayo yamesemwa leo na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Seif Shekalaghe kwa niaba ya Naibu Waziri Dkt. Godwin Mollel wakati wa maadhimisho ya siku ya sikoseli duniani ambayo kitaifa yamefanyika jijini Arusha.

Dkt. Shekalaghe amesema Serikali imeweka mikakati mbalimbali ya kupambana na ugonjwa huo ikiwa ni pamoja na kuanzisha kliniki katika Hospitali za wilaya, mikoa, Kanda na taifa hivyo wakati umefika kwa wagonjwa kutosafiri umbali mrefu kutafuta huduma hizo.

“Tunaweka mikakati Wizarani kuwa mwaka ujao wakati tunaadhimisha siku hii tutahakikisha changamoto ya kutafuta huduma umbali mrefu inakua haipo kwani kliniki za Sikoseli zitakua karibu za wananchi lakini pia NHIF kuhakikisha kuwa katika vile vitita huduma hizi zinaingizwa katika bima ya Afya ili waweze kupata huduma hii vizuri kwa sababu huu ni ugonjwa ambao watu wanaishi nao maisha yao yote”. Amesema Dkt. Shekalaghe.

Dkt. Shekalaghe ameongeza kuwa Tanzania ni nchi ya tano Duniani kwa kuwa na idadi kubwa ya watu wenye Sikoseli ambapo kila mwaka wanazaliwa watoto 11,000 na mpaka Sasa idadi ya watu wenye sikoseli ni 200,000 ambapo watu 5 mpaka 7 kati ya 100 waliopo chini ya miaka mitano hufa kwa sababu mbalimbali kutokana na madhara yanayosababishwa na Sikoseli.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha Dkt. Silvia Mamkwe ameitaka jamii kuondoa mila potofu juu ya ugonjwa wa Sikoseli badala yake wazingatie kufanya vipimo wakati wa kupata wenza ili kuepuka kuoana wote wakiwa na vinasaba vya Sikoseli vinavyofanana hali itakayosaidia kutozaa watoto wenye ugonjwa huo.

“Huwezi kujijua kama una ugonjwa huu bila kupima hivyo tukate hii cheni ya kuendelea kurithi kwa kupima, kwani Serikali peke yake haiwezi ni muhimu tukashirikiana na jamii kumaliza tatizo hili”. Amesema Dkt. Mamkwe.

Mmoja wa mashujaa wa Sikoseli ambaye ameishi na ugonjwa huo kwa miaka 44 Bi. Sanyu Singa amesema wao kama mashujaa wanakabiliwa na changamoto nyingi lakini kubwa ni elimu juu ya Sikoseli kutokuwepo katika jamii.

“Tunatamani elimu itolewe kwanzia majumbani ili tunaoishi nao weweze kutuelewa na wajue kuwa ugonjwa huu hauambukizwi kwa kugusana bali ni wa kurithi lakini pia mtusaidie huduma za kliniki ya sikoseli ziwepo maeneo yote ikiwemo vijijini”. Amesema Bi. Sanyu.



from MPEKUZI

Comments