Mkazi Wa Babati Ahukumiwa Miaka 20 Jela Kwa Kukutwa Na Nyama Ya Twiga Ikiwa Jikoni.


 Na John Walter-Babati
Mahakama ya wilaya ya Babati imemuhukumu miaka 20 jela mwanaume mmoja mkazi wa kijiji cha Vilima Vitatu wilayani humo Mashaka Issa Gway (41)  kwa kukutwa na nyara ya serikali.

Hukumu hiyo imetolewa  Juni 9,2022 baada ya mahakama kujiridhisha na ushahidi uliotolewa kwamba mtu huyo alikutwa na nyara hiyo ambayo ni Nyama ya Twiga yenye thamani ya shilingi Milioni 34.785.

Akisoma hukumu hiyo Mheshimiwa Hakimu wa mahakama ya wilaya ya Babati Victor Kimario, amesema Mashahidi wawili Kati ya Saba walitoa ushahidi ambapo Shahidi ambaye ni mtambuzi wa Nyama ya wanyamapori alithibitisha nyama hiyo ilikutwa kwenye Sinia ikiwa imepikwa mnamo Machi 23,2021 nyumbani kwake eneo la vilima vitatu.

Hata hivyo Mshtakiwa aliomba mahakama impunguzie adhabu kwa kuwa ana mke na watoto ambao wanamtegemea,ombi ambalo liligonga Mwamba.

Upande wa mashtaka ulieleza kuwa adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa Sheria ya uhifadhi wa wanyamapori namba 5,2009, Kifungu cha 86 (1) na (2) (b) inayosimama pamoja Sheria ya Uhujumu uchumi sura ya 200 marejeo ya mwaka 2009.

Amesema adhabu hiyo ni fundisho kwa wengine kwa kuwa Twiga ni kati ya wanyama watano wanaoiingizia pato serikali kupitia watalii wanaokuja nchini


from MPEKUZI

Comments