Na Munir Shemweta, WANMM DODOMA
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amekutana na wamiliki wa shule na vyuo visivyo vya kiserikali kujadili hoja ya wamiliki hao kutaka waondolewe kulipa kodi ya pango la ardhi kwa shule na vyuo hivyo.
Hatua hiyo inafuatia Shirikisho la Wamiliki wa Shule na Vyuo visivyo vya kiserikali (TOMONGSCO) kuwasilisha hoja kwa Waziri wa Ardhi ya kutaka ufafanuzi na kuondolewa kwa kodi ya pango la ardhi kwa maelezo kuwa shule na vyuo vinatoa huduma kama zinavyofanya shule za serikali.
Wakiwasilisha hoja zao mbele ya Dkt Mabula Juni 16, 2022 jijini Dodoma, wamiliki hao walisema, ni vizuri wao wakatambulika kama Taasisi zinazoisaidia serikali katika suala la zima la kutoa huduma ya elimu badala ya kutazamwa kama wafanyabiashara.
Katibu Mkuu wa Shirikisho hilo Benjamin Maduhu alisema, gharama zinazotumiwa kuhudumia wanafunzi wa shule na vyuo hivyo ni kubwa ukilinganisha na ada inayolipwa na wazazi na kuiomba serikali kuangalia namna bora ya kuwaondolea kodi ya pango la ardhi ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi.
‘’Mhe Waziri gharama za kodi ya pango la ardhi kwa shule na vyuo vyetu ni kubwa tunakuomba utusaidie iondolewe maana tunateseka sana na kuna wakati tunafikiria kubadilisha hata matumizi ziwe hoteli’’ alisema Maduhu.
‘’Serikali iangalie namna gani ya kutuondolea hii kodi ya pango la ardhi maana shule na vyuo visivyo vya kisrerikali vinatumia gharama kubwa kuziendesha na return yoyote ikianza kurudi basi ni almost ten years na baada ya hapo majengo yanahitaji kukarabatiwa’’ alisema mmoja wa wamiliki hao ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini Jesca Msavatavangu.
Wamiliki hao walieleza kuwa, wao na serikali siyo washindani lakini kwa kuwa wanaisaidia serikali kutoa huduma ya elimu hasa kwa wale wanafunzi wasiochaguliwa kujiunga na shule za serikali basi wangetamani serikali kuwatambua kama msaada na kuwaondolea kodi ya ardhi.
Akijibu hoja za wamiliki hao Waziri wa Ardhi Dkt Mabula alisema hoja zilizowasilishwa kwake ni lazima zipitiwe kwa kina na wataalamu kuona hoja za msingi na sheria na kuona kama upo umuhimu wa kuiondoa kodi hiyo kutokana na maombi yaliyowasilishwa kwenda kupunguza kodi ya serikali jambo alilolieleza lina mchakato mkubwa.
‘’Najua hamshindwi kulipa kodi ya ardhi bali siyo vipaumbele kwenu na ingekuwa kodi hiyo inaingizwa kwenye bili ya umeme au maji mgelipa, sisi hatuna uwezo wa kuwabana, Aidha mgelipia kwa wakati kodi hii wala msingehisi maumivu na mnaona ugumu kwa kuwa mmelimbikiza madeni na mtu anatakiwa kulipa milioni kumi anaona kubwa’’ alisema Dkt Mabula
Kwa mujibu wa Dkt Mabula, anachoweza kufanya kwa sasa kuhusu suala hilo ni kuzungumza na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt Mwigulu Mchemba kuangalia namna ya kuwaondolea riba kwa wale wanaodaiwa ili walipe kodi ya msingi na kuwataka wamiliki wanaodaiwa kulipa kodi ya pango la ardhi.
Wamiliki wa Shule na Vyuo visivyokuwa vya kiserikali walikwenda kumuona Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula kwa lengo la kupata ufafanuzi kuhusu tozo ya kodi ya ardhi kwa vyuo na shule hizo sambamba na kuwasilisha ombi la kutaka kuondolewa kabisa kodi hiyo..
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment