CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeiomba Serikali kuangalia namna bora ya kufufua na kukwamua mchakato wa Katiba mpya kwa maslahi mapana ya Taifa.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka ameyasema hayo Juni 22,2022 jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Shaka amesema, katika kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu walichokaa wamekubaliana suala la Katiba mpya liangaliwe kwa maslahi mapana ya Taifa.
Amesema,Halmashauri Kuu ya Taifa kwa kauli moja imekubaliana upatikanaji wa Katiba mpya na chama hicho kinakubaliana na umuhimu wa kupatikana izingatie mazingira ya sasa.
Pia akizungumzia masuala ya Uchaguzi Mkuu wa ndani ya chama,Shaka amesema Halmashauri Kuu ya Taifa imepokea na kuridhishwa taarifa ya maendeleo ya uchaguzi wa ndani ya chama ambao umeshakamilika kwa asilimia 99.5 katika ngazi ya mashina na matawi kote nchini na sasa upo katika ngazi ya kata na wadi.
Pia amesema kuwa, miongoni mwa mambo ambayo Halmashauri Kuu imeshauri kutazamwa ni pamoja na kesi zenye sura ya kisiasa kwa wafuasi na wanachama wa vyama mbalimbali vya siasa nchini.
Amesema, chama kimeishauri Serikali utekelezaji wa masuala yote ya kuimarisha demokrasia nchini na kutaka mazingira ya kisiasa yafanyike bila kuathiri uhuru na usalama wa nchi yetu.
Licha ya hayo ameeleza kuwa Halmashauri Kuu ya Taifa imempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa ukomavu, ustahimilivu, uhodari na dhamira yake njema ya kufanya maridhiano na vyama vya siasa nchini kwa lengo la kuimarisha umoja, ushirikiano, mshikamano, amani na utulivu kwa maendeleo na ustawi wa watanzania wote.
"Halmashauri Kuu ya Taifa imevipongeza vyama vyote vya siasa kwa kukubali kuunga mkono hatua hiyo, chama kimeishauri Serikali kuharakisha utekelezaji wa masuala yote yatakayojenga kuaminiana, kuimarisha ushirikiano na umoja wa kitaifa kwa ustawi wa wananchi wote,"amesema.
Vilevile Halmashauri Kuu ya Taifa imempongeza Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Husein Ali Mwinyi kwa kuendelea kuonesha uvumilivu na ukomavu wa kiuongozi katika kuongoza serikali ya umoja wa kitaifa, hali inayochochea umoja, amani na utulivu kwa wananchi wa Zanzibar na hivyo kuharakisha maendeleo yao.
Hayo yanajiri baada ya Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuongoza Kikao cha Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) iliyokutana leo Juni 22, 2022 katika Ukumbi wa White House makao makuu ya CCM jijini Dodoma ikiwa ni utaratibu wa vikao vyake vya Kitaifa.
Juni 21,2022 Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) iikutana Ikulu Chamwino, Dodoma kwa kikao cha siku moja cha kawaida na kufuatia kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa kilichofanya uchaguzi wa kujaza nafasi mbili za wajumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri ya Taifa zilizokuwa wazi kwa kuwachagua kwa kura Stephen Masatu Wassira na Theresia Adriano Mtewele.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa,Itikadi na Uenezi (NEC) Shaka Hamdu Shaka amesema, vikao hivyo vyote viwili vimejadili masuala mbalimbali ya msingi na kwamba pamoja na mambo mengine, Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM imefanya uteuzi wa wenyeviti wa halmashauri za wilaya na mameya.
Shaka amesema, uteuzi huo ni Halmashauri ya Wilaya ya Njombe Mji,Erasto B. Mpete,Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro,Mohamed Festo Bayo na Halmashauri ya Manispaa ya Moshi,Stuart Nathaniel Nkinda, Apaikunda Ayo Naburi na Zuberi Abdallah Kidumo.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment