China yawaasa viongozi wa Marekani wachunge kauli zao kuhusiana na Taiwan


China imetoa jibu kali dhidi ya uingiliaji wa waziwazi wa Marekani katika masuala ya ndani ya nchi hiyo. Beijing imewaasa viongozi wa Washington wachunge kauli wanazotoa kuhusiana na Taiwan.

Katika kile kinachoonekana kuwa ni uingiliaji wa masuala ya ndani ya China, Rais Joe Biden wa Marekani ambaye jana alikuwa ziarani nchini Japan alitangaza waziwazi uungaji mkono wake kwa Taiwan na kutamka kwamba: "ikiwa China itaishambulia Taiwan, Marekani itaisaidia na kuiunga mkono kijeshi Taiwan."

Akiwa mjini Tokyo, Biden aliongezea kwa kusema: "sisi tumetoa ahadi kuhusiana na Taiwan. Utumiaji wowote wa mabavu na ulazimishaji wa China dhidi ya Taiwan haufai na utachukuliwa kuwa ni kitu kisichokubalika. Kwa hatua zake, China inauathiri ukanda mzima na kitakachojiri hali sawa na iliyotokea Ukraine."

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China amejibu matamshi hayo ya rais wa Marekani kuhusiana na Taiwan kwa kusema: "kadhia ya Taiwan na Ukraine ziko tofauti kabisa; na si sahihi kuzilinganisha hata kidogo."

Zhao Lijian ameongezea kwa kusema: "Taiwan ni sehemu ya ardhi ya China na sisi hatuiruhusu nchi yoyote iingilie masuala yetu ya ndani."

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China amegusia pia kauli kali ya vitisho aliyotumia Joe Biden dhidi ya nchi yake na akasema:"Marekani inatambua kwamba China inao uwezo wa kulinda ardhi yake."

Serikali ya Beijing imekuwa ikisisitiza kuwa kadhia ya Taiwan haina chochote cha kulinganishwa na kinachoendelea Ukraine ikisistiza kuwa kisiwa cha Taiwan ni sehemu ya ardhi kuu ya China.

China imeshaionya Marekani mara kadhaa kwamba haitakuwa tayari kufanya maridhiano yoyote juu ya suala la Taiwan na itatoa jibu kali kwa chokochoko zozote zitakazofanywa juu ya suala hilo



from MPEKUZI

Comments