Sakata la usafiri wa bodaboda na bajaji kuingia Katikati ya Jiji la Dar es Salaam limetua bungeni baada ya Mbunge wa Ukonga (CCM), Jelly Silaa kulitaka Bunge kusimamisha shughuli zake na kujadili sakata hilo.
Hata hivyo, Spika wa Bunge, Dk Tulia Akson amesema hoja hiyo haiwezi kujadiliwa bungeni hapo na badala yake amemuomba Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kushughulikia jambo hilo.
Baada ya kipindi cha maswali na majibu leo Alhamisi Aprili 21, 2022 mbunge huyo ameomba kutoa hoja ya kuahirisha shughuli za bunge ili jambo hilo lijadiliwe amesema; “Ni muhimu sana kwa sababu bodaboda wanabeba kundi kubwa la nguvu kazi ya vijana”
"Mheshimiwa Spika, hata wewe juzi ulipokwenda Mbeya ulipokelewa na kundi kubwa la vijana wa bodaboda na maeneo mengine tunawategemea, Jijini Dar es Salaam kumekuwa na sintofahamu kuhusu kundi hili, naomba wenzangu waniunge mkono tulijadili," amesema Silaa.
Akijibu hoja hiyo, Spika Dk Tulia amesema ili hoja ijadiliwe lazima kiti chake kijiridhishe kuwa inafaa kuingia kwenye mjadala lakini kwa jambo hilo Serikali ibebe dhamana ya kulishughulikia.
"Kiongozi wa shughuli za Serikali Bungeni ambaye ni Mheshimiwa Waziri Mkuu yupo hapa tunaomba ulibebe jambo hili na kutoa mwongozo ikiwemo magari ya Kigoma, ili watu wajue," amesema Dk Tulia.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment