WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema kuwa Tanzania itandelea kuwa mstari wa mbele kuisaidia nchi ya Msumbiji katika kukabiliana na vitendo ya kigaidi katika nchi hiyo.
Ameyasema hayo jana (Alhamisi, Machi 24, 2022) alipomuwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan kwenye mkutano wa kujadili usalama katika eneo la Kusini Mashariki mwa Afrika hususan nchini Msumbiji na maeneo ya jirani (Aqaba Process), uliofanyika katika mji wa Aqaba uliopo nchini Jordan.
“Tanzania tutaendelea na ushiriki wetu wa kuisaidia Msumbiji kwa kiwango wanachohitaji, lengo ni kuhakikisha tunauondoa kabisa ugaidi nchini humo, tunapunguza hatari ya magaidi kuingia nchini Tanzania, pamoja na kuwasaidia kwa hali na mali wananchi wake kuendelea na shughuli zao”.
Amesema kuwa mkutano huo pia umepokea mapendekezo mbalimbali kutoka kwa Msumbiji na wadau wa Aqaba Process kuhusu namna ya kuimarisha ushirikiano na kuisaidia Msumbiji kukabiliana na changamoto za ugaidi.
Waziri Mkuu ameongeza kuwa “Eneo linaloshambuliwa ni Kaskazini mwa Msumbiji ambalo ni Kusini mwa nchi yetu, hivyo ushiriki wetu umekuwa ni muhimu sana”.
Mkutano huo ambao umeitishwa na Mfalme Abdullah II wa Jordan, utakuwa wa tatu kufanyika tangu kuanzishwa kwake mwaka 2015 na huwakutanisha viongozi wakuu wa nchi za ukanda wa Mashariki ya Afrika kwa lengo la kujadili changamoto za ugaidi na namna ya kuudhibiti.
Baadhi ya viongozi walioshiriki katika mkutano huo ni pamoja na Rais wa Msumbiji, Filipe Nyusi, Rais wa Rwanda, Paul Kagame na Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Felix Tshisekedi
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment