Na. Ramadhani Kissimba na Saidina Msangi – WFM Dodoma
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba amekutana na timu ya watalaam kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) ili kujadili namna ya kuendeleza ushirikiano katika kufuatilia miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo ilishaamuliwa kutekelezwa kati ya Serikali na Benki hiyo.
Dkt. Mwigulu alikutana na ujumbe huo ofisini kwake Jijini Dodoma na aliwashukuru Watalaam hao kwa kutekeleza maagizo yaliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dkt. Akinumwi Adesina, walipokutana mwezi Februari, 2022 Jijini Dodoma.
‘’Niwashukuru kuitikia maelekezo ya Viongozi wetu ambapo katika kikao chao walielekeza timu za watalaam zianze kukaa kujadiliana namna ya kukamilisha haya mazoezi mawili moja ni la kuangalia dirisha la Tanzania, kuongeza wigo wa kupata fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo na la pili ni katika kuendeleza ushirikiano katika miradi ambayo ilishaamuliwa’’. Alisema Dkt. Nchemba.
Dkt. Nchemba aliongeza kuwa dirisha hilo ni la muhimu kwa kuwa Tanzania tayari ilikuwa inatumia fedha hizo katika miradi ya miundombinu kama vile barabara, nishati pamoja na huduma za jamii.
Alisema kuwa nchi inatarajia kuwa mgao wa fedha hizo utaongezeka kutoka takribani dola milioni 250 za sasa hadi dola milioni 750 zitasaidia katika kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo ambayo ipo katika dira ya Taifa na dira ya Kiongozi, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Dkt. Nchemba ameuhakikishia ujumbe huo kuwa Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na Idara zote za Serikali wapo tayari kutoa ushirikiano kama Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan alivyoelekeza na pia Wizara ipo tayari kutoa ushirikiano wa upatikanaji wa mahitaji ya takwimu pamoja na maelezo ya kisera na kimkakati ambayo yatayokuwa na umuhimu katika kufanya uamuzi ili kuharakisha utekelezaji wa majukumu hayo.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dkt. Victoria Chisala, alisema kuwa Benki inaendelea na utaratibu wa kuongeza wigo wa dirisha la Tanzania katika kupata fedha za kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo na taarifa rasmi zitatolewa na kuongeza kuwa fursa ya kuongezewa dirisha la AfDB inatokana na uwezo wa nchi wa kuongeza rasilimali ambapo Tanzania ina uwezo huo.
Dkt. Nchemba aliutaka ujumbe huo, mara watakapokamilisha majadiliano hayo kutembelea vivutio mbalimbali vya Utalii vilivyopo nchini hasa Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro na Visiwa vya Zanzibar kwa kuwa Ngorongoro na Zanzibar ni maeneo ambayo hayafanani na eneo lolote duniani.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment