Na Dotto Mwaibale, Singida
WAZIRI wa Madini Dk.Doto Biteko anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kongamano la madini litakalofanyika Februari 19, 2022 wilayani Iramba mkoani Singida.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Wilaya ya Iramba Suleiman Mwenda wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kongamano hilo ambalo litaongeza chachu ya maendeleo katika wilaya hiyo kupitia sekta ya madini.
” Kongamano ili ni fursa kubwa kwetu Wana Iramba kwani kutakuwa na mada mbalimbali zitakazohusu masuala ya madini ambayo tunayachimba kwa wingi hapa wilayani kwetu” alisema Mwenda.
Aidha Mwenda alisema kongamano hilo litatanguliwa na maonyesho yenye lengo la kutangaza fursa za madini wilayani Iramba na kuongeza shughuli za uchimbaji madini.
Alisema ofisi yake kwa kushirikiana na wadau wa madini wilayani humo,taasisi za fedha,mashirika ya umma na yasiyo ya kiserikali wanawa karibisha wadau wote katika kongamano hilo ambalo ni la muhimu litakalofanyika Jumamosi kwenye ukumbi mkubwa wa Halmashauri hiyo uliopo mjini Kiomboi.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment