Na. Saidina Msangi, WFM, Dodoma
Serikali imesema kuwa inatekeleza sera na mikakati mbalimbali kupitia Benki Kuu ya Tanzania ili kuhakikisha kuwa riba za mikopo zinashuka ili kuwezesha makundi yote likiwemo kundi la vijana kupata mikopo yenye riba nafuu na kuweza kushiriki vyema katika shughuli za kiuchumi.
Hayo yameelezwa bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), alipokuwa akijibu swali la Mheshimiwa Lucy John Sabu, Mbunge wa Viti Maalum, aliyetaka kujua Serikali ina mpango gani wa kuweka dirisha maalum la vijana kwenye kila benki za Serikali nchini ili kuwezesha vijana kupata mahitaji na mikopo yenye riba nafuu.
“Kwa sasa Benki za Serikali zinatoa huduma za mikopo kwa makundi yote likiwemo kundi la vijana kwa kuzingatia taratibu za utoaji mikopo za mabenki ambapo kwa wale wenye vigezo hupatiwa mikopo bila usumbufu wowote”, alisema Mhe. Chande.
Alisema Serikali itaendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kuhakikisha vijana wote wanaokidhi vigezo na masharti ya kupata mikopo wanapatiwa mikopo ili kuendesha shughuli zao na hatimaye waweze kuwa na mchango kwenye ukuaji wa uchumi na pato la taifa.
Mhe. Chande aliongeza kuwa Serikali ilianzisha Programu Maalum ya utoaji mikopo ya uwezeshaji yenye riba nafuu kwa Vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu wenye ulemavu ambapo Halmashauri zote zinatakiwa kutenga asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa ajili ya kutoa mikopo kwa makundi hayo.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment