Na WMJJWM – Mwanza
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima amesema kuwa, moja ya sababu ya Watoto kukimbia nyumbani na kuishi mitaani ni ukosefu wa Malezi bora kwa Watoto hivyo, uzinduzi wa Kituo cha Malezi na Makuzi Soko la Mirongo kikawasaidie na kuwa suluhisho.
Waziri Dkt. Gwajima ameyasema hayo wakati akizindua Kituo cha Malezi na Makuzi kwa watoto wadogo katika soko la Mirongo Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza chenye lengo la kuwasaidia wafanyabishara wanawake wenye Watoto kuwaweka Watoto wao wanapokuwa wanaendelea na biashara zao.
Dkt. Gwajima amesema kuwa jukumu la Malezi na Makuzi kwa watoto ni la wazazi nyumbani hivyo amewataka wazazi kuzingatia suala la Malezi ili kupunguza changamoto mbalimbali zinaowapata Watoto hasa vitendo vya ukatili.
“Suala la Malezi na Makuzi kwa watoto ni muhimu kwa ukuaji na maendeleo na Ustawi wa kundi hilo katika kujenga Taifa lenye watu wenye Afya uzalendo na uwajibikaji” alisema Dkt. Gwajima
Ameongeza kuwa Wizara yake itahakikisha inaratibu wadau mbalimbali ili huduma ya Malezi na Makuzi kwa watoto katika Vituo vya kulelea Watoto wadogo iweze kuifikia jamii kwa urahisi.
Aidha Dkt. Gwajima amesema azma ya Rais Samia ni kuona Mipango na mikakati mbalimbali ya Serikali inaifikia Jamii ikiwemo Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto ili kupmaba na vitendo vya ukatili nchini.
Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mwanza ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Amina Makilagi amesema kuwa, Mkoa wa Mwanza unaendelea kuhakikisha watoto wanapata haki na huduma stahiki ikiwemo Malezi na Makuzi kwao.
“Mhe. Waziri wewe umekuwa Waziri wa ajabu sana, pengine ungeweza kukaa Ofisini, lakini wewe umeamua kushuka huku chini na kuja kuongea na Kamati za (MTAKUWWA), kwakweli nikiri umetupatia funzo kubwa sana” amesema Makilagi.
Awali Naibu Katibu Mkuu. Ndugu Amoni Mpanju, alisema, kuanzishwa kwa Wizara maalum ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi Maaalum ni hatua kubwa kwa nchi na Maono ya Mhe. Rais hivyo lazima Watendaji waelewe na wafanikishe ndoto na maono ya Mhe Samia.
Akizungumza katika hafla ya Uzinduzi wa Kikao hicho, Mkurugenzi wa Shirika la Kivulini Yassin Ali amesema, Shirika lake litaendelea kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha wafanyabiashara wanawake wenye watoto wadogo kupata sehemu ya kuwakabidhi watoto wao wakati wakiwa katika majukumu ya kazi.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment