Tanzania Yapokea Msaada Wa Dawa, Vifaa Tiba Kutoka Nchini Misri


Na. Wizara ya Afya – Dar es Salaam

Serikali kupitia Wizara ya Afya imepokea msaada wa dawa pamoja na vifaa tiba vyenye thamani ya Tsh: Mil. 864 vitavyosaidia katika kupambana dhidi ya magonjwa mbalimbali kutoka katika Serikali ya Misri.

Msaada huo umetolewa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es salaam kupitia kwa Balozi Misri nchini Tanzania Mhe. Mohamed Gaber Abouelwafa na kupokelewa na katibu Mkuu Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi kwa niaba ya Mhe. Ummy Mwalimu, Waziri wa Afya.

Akipokea msaada huo, Prof. Makubi amesema, msaada huo umeletwa baada ya ziara ya kikazi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kutembelea nchini Misri mnamo mwezi November mwaka jana (2021).

“Tunamshukuru sana Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Tanzania pamoja na Serikali ya Misri kwa kushirikiana na Tanzania hasa katika kuboresha Sekta ya Afya kwa kusaidia mahitaji mbalimbali ikiwemo upatikanaji wa dawa na vifaa tiba.”Amesema Prof. Makubi.

Aidha Prof. Makubi amesema msaada huo utaenda kuwasaidia wananchi wenye uhitaji katika vituo mbali mbali vya kutolea huduma za afya nchini.

Kwa upande wake Balozi wa Misri nchini Tanzania Mohamed Gaber Abouelwafa amesema kujitoa kwa Serikali ya Misri, kusaidia Sekta ya Afya ni kutokana na jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan katika kuwaletea maendeleo wananchi, ikiwemo kuboresha Sekta ya Afya nchini kwa kupambana dhidi ya magonjwa.

“Serikali ya Misri itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kusaidia Maendeleo ya Watanzania, hasa katika kuboresha Sekta ya Afya, hii inatokana na nia njema ya Mhe. Rais Samia katika kuleta maendeleo kwa wananchi, hususan katika kuboresha Sekta ya afya.” Amesema Mhe. Balozi Abouelwafa.

Kwa uongozi makini chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, Serikali ya Misri imetoa ahadi kuendelea kusaidi Sekta ya Afya nchini kwa kuendelea kuleta Dawa pamoja na vifaa tiba kwaajili ya kupambana dhidi ya Magonjwa mbalimbali.



from MPEKUZI

Comments