NATO kupeleka wanajeshi wa ziada Ulaya Mashariki

 Jumuiya ya kujihami ya NATO imesema, inawaweka tayari wanajeshi wake ziada na kupeleka meli zaidi pamoja na ndege za kivita Ulaya Mashariki.


Hatua hiyo imekuja wakati Ireland ikitahadharisha kwamba luteka mpya za kijeshi za Urusi nje ya pwani yake hazikubaliki kutokana na mivutano iliyopo kuhusu suala la madai kwamba rais Vladmir Putin analenga kuishambulia Ukraine.

Katibu mkuu wa NATO Jens Stoltenberg amesema jumuiya hiyo inachukuwa hatua zote zinazostahili kulinda na kuwatetea washirika wake wote. 

Jumuiya hiyo imesema inaimarisha uwepo wa jeshi lake katika eneo la bahari ya Baltic wakati Denmark ikipeleka ndege za kivita nchini Lithuania na Uhispania nayo ikitangaza pia itapeleka meli za kivita na pengine ndege za kivita nchini Bulgaria. Aidha Ufaransa imesema inajiandaa kupeleka wanajeshi nchini Bulgaria.

Hatua hizo zimetangazwa wakati mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za Umoja wa Ulaya wamekutana kuonesha msimamo wa pamoja wa kuiunga mkono Ukraine na kuondowa mashaka yaliyokuwepo juu ya migawanyiko kuhusu namna ya kuukabili uchokozi wa Urusi.




from MPEKUZI

Comments