Na. WAF- Morogoro
Katibu Mkuu Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi amewataka Waganga Wakuu wa Mikoa na Waratibu wa Chanjo ngazi za Mikoa na Wilaya kuwa na ushawishi kwa wananchi ili kujitokeza kwa wingi kupata huduma ya chanjo dhidi ya UVIKO-19.
Prof. Makubi ameyasema hayo tarehe 23/1/2022 alipokuwa akifunga mkutano wa tathmini ya huduma za chanjo ngazi ya Mikoa/Wilaya uliofanyika kwa siku Tatu katika manispaa ya Morogoro.
“Niwaombe sana Waganga Wakuu wa Mikoa mkawe na ushawishi mzuri, chanjo zisiwe zinabaki Mikoani au wilayani mkazitoe kwa kuwapatia wananchi huduma.”amesema Prof. Makubi
Aidha, Prof. Makubi amesisitiza kuwa na uwajibikaji mzuri kazini kwa kuwa baadhi ya watendaji hawafanyi vizuri katika uongozi wao.
“Kuna baadhi ya viongozi hamfanyi vizuri, mkajirekebishe Kuna malalamiko kutoka kwa wadau mbalimbali juu ya utendaji wenu.”Almesisitiza Prof. Makubi
Amesema Serikali inajitahidi kutoa sapoti kwa kutoa vifaa na fedha ili watendaji wakafanikiwe katika kutekeleza majukumu yao ya kazi.
Pia amesema ombi la Waratibu hao wa chanjo wa Mkoa/Wilaya kuwapatia usafiri wa pikipiki litafanyiwa kazi ili kurahisisha majukumu yao ya huduma tembezi za chanjo na zile za kila siku katika maeneo yao ya kazi. Kwa sasa tayari Serikali ya awamu ya Sita chini ya Mhe Rais Samia Suluhu Hassan umenunua magari zaidi ya 200 kwa ajili ya waganga Wakuu Wilaya Wote nchini.
Hata hivyo Prof. Makubi ameipongeza Mikoa inayofanya vizuri katika uchanjaji wa UVIKO-19 ikiwemo Ruvuma, Mara na Mwanza. “Naagiza mikoa mingine kujifunza mbinu na mikakati iliyotumika kwenye mikoa hii ili waweze kuitumia kuleta mafanikio katika mikoa yao.”amesema Prof. Makubi
Malengo ya mkutano huo yalikuwa ni kupitia taarifa za utekelezaji wa huduma za chanjo kwa mwaka 2021, kutambua mafanikio na changamoto na kuweka mipango ya kuboresha zaidi huduma za chanjo kwa mwaka 2022.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment