Meseji za Mbowe kesi ya ugaidi Zasomwa Mahakamani

Jumbe fupi za maneno (meseji), zinazodaiwa kuwa za Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na baadhi ya washtakiwa wenzake, katika kesi ya ugaidi inayowakabili, zimesomwa kwenye Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Dar es Salaam.
 

Meseji hizo zinazodaiwa kutumwa katika mitandao ya kijamii ya Telegram na WhatsApp, zimesomwa  Jumanne, tarehe 18 Januari 2022 na Mchunguzi wa Kitengo cha Uchunguzi wa Kisayansi cha Jeshi la Polisi, Inspekta Innocent Ndowo wakati akitoa ushahidi wake mahakamani hapo, mbele ya Jaji Joachim Tiganga.

Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine katika kesi hiyo yenye mashtaka ya ugaidi, ni waliokuwa makomandoo wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Halfan Bwire Hassan, Adam Kasekwa na Mohammed Abdillah Ling’wenya.

Shahidi huyo wa 10 wa Jamhuri, amesoma meseji hizo baada ya kukabidhi mahakamani hapo taarifa za uchunguzi wa kisayansi za simu, alioufanya kwenye simu zinazodaiwa kuwa za kina Mbowe.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Pius Hilla, Inspekta Ndowo, alianza kusoma mawasiliano yanayodaiwa kufanyika kati ya Julai hadi Agosti 2020, katika mtandao wa Telegram, kati ya namba inayodaiwa kuwa ya Mbowe, na  inayodaiwa kuwa ya Denis Urio.

Kwa mujibu wa ushahidi wa Inspekta Ndowo, meseji hizo zinaonesha namba za Mbowe alizotumia kuwasiliana na Urio, kwa ajili ya kumtafutia watu wa kumfanyia kazi pamoja na namna alivyotumia fedha za kufanikisha zoezi hilo.

Ushahidi uliowahi kuletwa mahakamani hapo na Jamhuri, unadai kuwa Mbowe alimuomba Urio amtafutie waliokuwa makomandoo wa JWTZ, kwa ajili ya kumsaidia kupanga njama za vitendo vya kigaidi, ambapo inadaiwa alitoa zaidi ya 600,000 kufadhili mipango hiyo.

Inspekta Ndowo alisoma mawasiliano hayo kama ifuatavyo;

Kuanzia tarehe 20 Julai 2020, muda wa saa 1 asubuhi, mmiliki wa kielelezo hiki (Urio), kupitia akaunti ya Telegram alipokea ujumbe kutoka kwa mmiliki wa Telegram ambayo ni ya namba ya Free (Mbowe), ujumbe unasema, “kaka wale mtu tatu au nne ni muhimu sana na siku zimekwisha.”

Inspekta Ndowo aliendelea kusoma, akidai siku hiyo hiyo Free alipiga simu kwa kielelezo hicho (Urio), wakaongea sekunde 54. Mnamo siku hiyo hiyo saa 1 asubuhi wakaongea duration (kipindi) ya sekunde 55.

Tarehe 20 Julai 2020, muda wa saa 2 asubuhi kupitia Telegram, Urio alituma ujumbe kwenda kwa Free, ambao unasomeka “Broo kuna members wawili hadi sasa, mmoja yuko Tunduma anafanya kazi katika kampuni inayosafirisha magari nje ya nchi na mmoja anafanya kazi zake.”

Tarehe 20 Julai 2020, muda wa saa 2 asubuhi, Urio anadaiwa kutuma meseji “sio salama sana niwezeshe.” Tarehe hiyo hiyo kuna ujumbe kutoka kwa Urio kwenda kwa Free uliosomeka “kikubwa ilikuwa hizo shughuli wanazofanya waziache, sasa hivi waje waelekezwe.”

Inspekta Ndowo aliendelea kusoma meseji hizo akidai, siku hiyo hiyo saa 2 asubuhi, Free alituma ujumbe katika kielelezo hicho (Urio), unaosema “hao wawili kwa kuanzia sio mbaya wanaweza kuelekezwa kuwa na mimi full time, wamekwambia wanataka nini na una maoni gani.” Saa 2 asubuhi Free alituma tena ujumbe uliosema ” sema tu kaka nitasemaje.”

Inspekta Ndowo alidai, siku hiyo muda wa saa 2 asubuhi, Urio alituma ujumbe kwenda kwa Free, unaosomeka “mmoja kazaliwa 1984 na mwingine 1986.”

Kwa mujibu wa Inspekta Ndowo, siku hiyo hiyo asubuhi, Urio alituma ujumbe kwenda kwa Free, unaosema “naomba unitumie nauli kumobilize kwenda nao Moro.” Ambapo Free alijibu akidai “no problem kaka, kiasi gani na kwa simu ipi.”

Urio alijibu ujumbe huo akisema “500,000.” ambapo Free alijibu akisema “sawa kaka tayari.

Inspekta Ndowo aliendelea kusoma akidai, Urio alimtumia Free ujumbe uliosomeka “nashukuru nimeupata, nitakupa majibu jioni.” Urio alituma tena meseji kwa Free iliyosomeka “usiwe unatumia namba binafsi kutuma pesa, tumia wakala au wasaidizi wako.” Ambapo Free alijibu “ok.”

Inspekta Ndowo anadai kuwa, kesho yake tarehe 21 Julai 2020, muda wa saa 5 asubuhi, Urio alituma ujumbe mwenda kwa Free, unaosomeka “shikamoo bro, habari ya kuamka.” Kisha akatuma tena “jamaa anayefanya kazi Yard ameshafika ninafanya mazungumzo naye.”

Shahidi huyo wa Jamhuri, amedai siku hiyo hiyo Urio alituma ujumbe mwingine kwenda kwa Free, uliosomeka “yule wa Tunduma yuko njiani anakaribia kufika Moro. Ila nina maswali wanayouliza kuhusu utawala, malazi yakatakuwaje pamoja na mshahara wao.”

Siku hiyo hiyo ya tarehe 21 Julai 2020 muda wa saa 2 jioni, Inspekta Ndowo anadai Urio alituma ujumbe kwenda kwa Free ukisema “Mkuu.”, kesho yake 22 Julai 2020 alimtumia tena meseji “mkuu shikamoo, habari ya asubuhi.” Alituma tena “vipi maendeleo ya mgonjwa wako.”

Urio alimtumia tena Free ujumbe “shikamoo mkuu, vijana wako tayari tunasubiri maelekezo yako. Nimekutana nao wote wako… niko nao na wako tayari kwa kazi.”

Siku hiyo hiyo, Urio alimtumia ujumbe Free akisema “naomba unipe utaratibu wao.” Ambapo Free alimjibu akisema “naendelea vizuri kaka.”

Inspekta Ndowo aliendelea kusoma meseji hizo akidai, Urio alituma meseji “wamekuja Dar, naomba uwatumie nauli na wapi watakapofikia.”

Inspekta Ndowo amedai, tarehe 22 Julai 2020, Free alituma ujumbe kwa Urio unaosomeka “kwa maana ya Sh. ngapi” kisha akatuma tena “tutakuwa na safari ya kwenda Hai leo usiku au kesho asubuhi.”

Shahidi huyo wa Jamhuri amedai kuwa, siku hiyo hiyo Urio alituma ujumbe kwenda kwa Free, uliosema “nauli na pesa ya kula 200,000 kwa wote wawili. Hakuna shida wako tayari.” Free anadaiwa kujibu ujumbe huo akisema “natuma kwa namba gani?” Urio alijibu akiandika namba “0787555200”.

Free alimjibu akisema “ni namba ya nani.” Urio alijibu akisema “namba yangu.” Baadae Urio alimtumia ujumbe Free uliosema “niliwatumia juzi. Lakini wewe usitumie namba yako” Free akajibu “ok”.

Inspekta Ndowo amedai kuwa, siku hiyo hiyo Free alituma ujumbe mwingine uliosema “wakiwa around Mlandizi watumie WhatsApp, wapo na basi gani? Wanafika Dar es Salaam saa ngapi, nitatuma gari kuwapokea Ubungo.”

Urio alimtumia ujumbe Free uliodai “niwape namba gani ili muweze kuwasiliana, ya WhatSApp.” Baadae akatuma tena “bado vijana wako safarini.” Ambapo Free akajibu ” namba ninayokutumia fedha ni ya dereva wangu wamtafuta yeye, yeye ndiye mwenyeji atakayewapokea.” Urio akajibu “Ok. Sawa nitumie hiyo namba ya driver.” Kisha akatuma tena “tayari mashukuru nimepata.”

Inadaiwa kuwa, Free alituma ujumbe “namba niliyotuma fedha.” Ambapo Urio akajibu “nashukuru nimeelewa nitawapa hiyo namba.” Mbowe alijibu “hope wameondoka.”

Siku hiyo hiyo muda wa saa 12 jioni, Urio alituma ujumbe “Yah tayari wameshaondoka, wanakaribia Ruvu sasa.”

Denis aliendelea kumtumia ujumbe Free uliosomeka “wale vijana wengine watatu nimewapata, Mwanza, Dodoma na Pwani. Ndio wako njiani.” Alituma tena ujumbe “nilikuwa naomba ushauri kama ikikupendeza uwe unanitumia pesa ya kutosha kuwa mobilize na kuwaleta. Hao wawili wako tayari hata kusafiri usiku.”

Inspekta Ndowo anadai kuwa, tarehe 22 Julai 2020 muda wa saa 2 usiku Urio alimpigia simu Free, kisha Free akatuma meseji “bado niko kamati kuu, tuma meseji please.” Kisha Urio akajibu “kuna msg nilizokutumia kuhusu wale vijana wengine ambao wako tayari.”

Kesho yake tarehe 23 Julai 2020, Urio alituma ujumbe kwa Free uliosomeka “naomba ujibu msg zanghapo juu za jana usiku.” Tarehe 24 Julai 2020, kisha akatuma tena “shikamoo mkuu, habari ya jioni. Wale vijana walishaondoka ni matumaini yangu kuwa kuna mtu wa kuwapokea.” Free alijibu “helo Bro nilishindwa kupokea simu yako, naamini umenielewa.”

Mbali na meseji hizo zinazodaiwa kuwa za Mbowe kwenda kwa Urio, Insepkta Ndowo alisoma meseji za Ling’wenya na Urio, zilizotumwa kupitia mtandao wa WhatsApp, kama ifuatavyo;

Tarehe 23 Julai 2020, muda wa saa 1 jioni baadhi ya ujumbe unaosomeka kuwa ni wa Mohammed uliotumwa kwa Urio kutoka kielelezo hicho ulisomeka hivi,” mbona hujatuma majina na picha ya Adam.” Ambapo alijibu kwa kutuma picha ya mwanaume na ujumbe uliosomeka Adam Kasekwa.

Siku hiyo hiyo, muda wa saa 1 usiku, Mohammed alituma ujumbe kwenda kwa Urio uliokuwa na picha yake.

Tarehe 24 Julai 2020, Mohammed alimtumia ujumbe Urio uliosomeka “bro kwema”, kisha Urio akajibu “poa dogo niaje, uko poa?”.

Siku hiyo hiyo, inadaiwa Mohammed alimtumia ujumbe Urio uliosema “mambo?” Ambapo alijibiwa “fresh, mambo yaanaendaje” Mohammed akajibu “Mungu anasaidia mpaka sasa hakuna mbaya bro.”

Urio aliendelea kumtumia ujumbe uliosomeka “hakuna lolote kutoka kwa hao jamaa.” Mohammed akajibu “tumeongea kuhusu malipo ya kuajiriwa ila bado hayajakamilika.”

Kisha Urio akajibu “yaani mlivyoongea mlikubaliana nini na kwa muda gani.” Mohammed alijibu “alidai katuajiri kabisa na mshahara kila mwezi.”

Baada ya kusoma mawasiliano hayo, Inspekta Ndowo aliiomba mahakama hiyo izipokee simu nne kati ya nane alizozifanyia uchunguzi, kama sehemu ya ushahidi wake ambapo Jaji Tiganga alizipokea.

Shahidi huyo anaendelea kutoa ushahidi wake.

Mohammed na mwenzake Kasekwa, walikamatwa tarehe 5 Agosti 2020, maeneo ya Rau Madukani, Moshi mkoani Kilimanjaro.

Mbowe na wenzake wanakabiliwa na mashtaka sita ya ugaidi, ikiwemo ya kupanga njama za ugaidi, kudhuru viongozi wa Serikali akiwemo aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya. Pia wanadaiwa kutaka kulipua vituo vya mafuta na maeneo yenye mikusanyiko ya watu, ili kuonesha Serikali imeshindwa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2020.

Credit: Mwanahalisi



from MPEKUZI

Comments