Mawaziri watakiwa kutenga muda wa kujitathmini binafsi na kikazi


Makamu wa Rais wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango amewataka viongozi wakiwemo mawaziri na naibu mawaziri kujifanyia tathmini ya utendaji kazi wao kila baada ya kipindi fulani.

Amewataka kufanya hivyo ili kuweza kubaini ni wapi wanafanya vizuri na wapi panahitaji marekebisho katika kuwahudumia wananchi.

Amesema pasipo kufanya hivyo watakuwa wakifanya kazi kwa mazoea na kushindwa kutatua kero zinazowakabilia wananchi ambao ndio waliowachagua.

Dkt. Mpango ametoa rai hiyo katika kikao maalum cha Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan na mawaziri na naibu mawaziri kilichofanyika jijini Dodoma siku chache baada ya viongozi hao kuapishwa kufuatia mabadiliko ya baraza la mawaziri.

“Mtenge muda wa kutafakari juu ya maisha yenu na kazi zenu…untafakari, hivi perfomance [utendaji] yangu mimi waziri… nimefanikiwa wapi, nimekosea wapi, wapi naweza nikaboresha zaidi,” amesisitiza Dkt. Mpango.

Pia ametumia jukwaa hilo kuhimiza vitendo vya nidhamu kwa viongozi na kuepuka majungu, rushwa, uchawi, rushwa ya ngono au ya aina yoyote kwani vinaharibu haiba ya uongozi.

Pamoja na hayo amewataka kuwaheshimu wasaidizi na viongozi wengine walio chini yao kwani kwa kufanya hivyo wanapata thawabu na kujenga mazingira mazuri ya kufanyia kazi.



from MPEKUZI

Comments