Bashungwa Atoa Agizo Kwa Wakuu Wa Mikoa Na Wilaya Kusimamia Usafi Wa Mazingira Ya Barabara


WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Innocent Bashungwa amewaagiza Wakuu wa Mikoa pamoja na Wakuu wa Wilaya nchini kuhakikisha wanasimamia suala zima la usafi katika barabara na  katika miradi yote ya barabara inayoendelea kujengwa hatua aliyosema itasaidia kuboresha wa barabara hizo.

Amesema haipendezi kuona barabara zilizojengwa kwa gharama kubwa ya fedha zikiwa chafu huku akitaka elimu iendelee kutolewa zaidi kwa wananchi hatua itakayosaidia kuondokana na tatizo hilo.

Bashungwa ameyasema hayo  Dar es Salaam leo wakati akipokea taarifa ya  utekelezaji wa miradi mbalimbali ukiwemo mradi wa kuendeleza Miji Mkakati (TSCP)mradi wa Ukuzaji na Uboreshaji wa Miji (ULGSP) na Mradi wa Uboreshaji na Uendelezaji wa Jiji la Dar es Salaam(DMDP) kutoka kwa kikosi kazi kinachosimamia miradi hiyo inayotekelezwa kwa fedha za mkopo kutoka Benki ya Dunia na kusimamiwa na Wakala wa barabara za mijini na vijijini(TARURA).

Aidha Bashungwa amezitaka Halmashauri zote nchini kuandaa ‘Mpango Kabambe’ wa uandaaji wa miji hatua itakayowezesha kuepukana na ulipaji wa fidia wakati wa ujenzi wa miradi mbalimbali itakayokuwa ikitekelezwa nchini.

Ameongeza kuwa kutokana na kasi ya Serikali katika ujenzi wa miradi mbalimbali nchini, kuna kila haja kwa Halmashauri kuharakisha mipango hiyo ili kushindana na kasi ya wananchi ya kufanya ujenzi inayoendelea katika miji mbalimbali.

” Ni vyema mkaharakisha utarataibu wa kuwa na ‘Master Plan’  hii itasaidia kupunguza uwezekano wa serikali kulipa fidia kwa wananchi pindi inavyotaka kujenga mradi wowote,” Amesema Bashungwa.

Lazima Serikali itangulie mbele ya mipango ya wananchi, kwa kuipanga miji mapema ili wananchi wakute mpango wa matumizi bora ya ardhi hiyo hatua ambayo baadae itaepusha kutokea kwa athari yeyote ya kiuchumi au kisaikolojia kwa wananchi.



from MPEKUZI

Comments