Waziri Makamba Asisitiza Kuongeza Kasi Ya Uzalishaji Wa Vifaa Vya Umeme, Akipongeza Kiwanda Cha Africab
KATIKA kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji na umeme katika vitongoji vyote nchini Waziri wa Nishati, January Makamba amewataka wawekezaji kuendelea kujitokeza na kuwekeza katika viwanda vya vifaa vya kuunganisha umeme ili kufanikisha lengo la Serikali la kutumia bidhaa za ndani katika utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini.
Akizungumza baada ya kutembelea kiwanda cha nyaya cha Africab kilichopo Kurasini jijini Dar es Salaam, akiwa ameambatana na Naibu Waziri Stephen Byabato Makamba amesema viwanda vya namna hiyo ni muhimu na vinahitajika zaidi ili kupunguza utegemezi wa vifaa kutoka nje ya nchi.
Aidha amesema mpango wa Serikali kwa sasa ni kuhakikisha Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inasambaza umeme katika vitongoji vyote nchini na hiyo ni baada ya kufanikiwa kupeleka umeme kwenye vijiji.
“Tuna vitongoji 64000 kati ya hivyo 37,000 bado havijafikiwa na huduma ya umeme......Tumedhamiria katika kipindi cha miaka minne chini ya uongozi thabiti wa Rais Samia Suluhu Hassan vitongoji hivyo lazima vifikiwe na huduma hiyo, na kwa kufanikisha hilo inatupasa tuhakikishe tuna vifaa vya kutosha vyenye ubora, nimefarijika baada ya kutembelea kiwanda hiki kinafanya kazi nzuri sana.''
Waziri Makamba amesema zinahitajika nyaya zenye kukidhi kilomita 340,000 kwa vitongoji vyote pamoja na vifaa vingine kama mita, transfoma na vifaa vingine vya umeme.
Vilevile Waziri Makamba amesema, zitahitajika transoma 38, 000 zaidi na kutumia wasaa huo kuwakaribisha wawekezaji wengi zaidi kuja na kuwekeza zaidi kwenye eneo hilo ili kuhakikisha vifaa vinapatikana nchini pamoja na kutengeneza ajira kwa wazawa.
“Nimeshuhudia uzalishaji unaoendelea hapa ila bado tunahitaji kuongeza, nimefurahi kuna mpango wa kuongeza kiwanda na niwaombe wawekezaji wengine wasisite kujitokeza na kuwekeza katika sekta hii ya Nishati.'' Amesema.
Kwa upande wake Meneja Masoko wa Africab, David Tarimo amesema kiwanda hicho kina uwezo mkubwa wa kuzalisha vifaa na kwa kutambua ukubwa wa uhitaji wameongeza uwekezaji kwa kufungua kiwanda kingine katika eneo la Kimbiji.
“Kuna kiwanda kingine tumeanzisha kule Kimbiji ili kuongeza uzalishaji na tutaendelea kuhakikisha tunazalisha bidhaa zetu katika ubora unaohitajika sokoni pamoja na kutoa ajira kwa vijana wa kitanzania.''
Tarimo ameishukuru Serikali kwa kuendelea kushirikiana nao na kuiomba iendelee kuweka mkazo wa matumizi ya bidhaa za ndani hasa katika kuhakikisha ubora wa utekelezaji wa miradi mbalimbali kwa kuwa Tanzania kwa sasa ina uwezo na hakuna sababu ya kuruhusu bidhaa nyingi ziingie kutoka nje ya nchi.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment