Waziri Gwajima Awaongoza Wataalam Wa Afya Kufatilia Suala La Vifo Vya Mama Na Mtoto


Na WAMJW, DODOMA
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsi, Wazee na Watoto Dkt.Dorothy Gwajima ameongoza kikao cha wataalamu wa afya hapa nchini wakiwemo Madakitari Bingwa,Waganga Wakuu wa Mikoa,Wilaya na Hospitali zote kikihusisha kamati ya kitaifa ya kufuatilia vifo vya wazazi vinavyotokea kila siku kwa ajili ya kujadili na kuchambua taarifa za vifo vilivyotokea tarehe 20 hadi 21/12/2021 kutokana na sababu za uzazi.

Kikao hicho kilichofanyika kwa njia ya mtandao wa TEHAMA ambapo Dkt Gwajima ameongoza kikao hicho kama sehemu ya mkakati wa Wizara ya Afya kuhakikisha kila kifo cha mzazi na mtoto mchanga kinafanyiwa tathimini ya kitaifa ndani ya saa 24.

Kufuatia kikao hicho Mojawapo ya vituo vilivyoripoti vifo kwa siku ya leo ni pamoja na Zahanati ya Songambele, Halmashauri ya Buhigwe Mkoa wa Kigoma ambapo Dkt. Gwajima amempongeza Muuguzi Nyanduni Joachim na timu yake kwa kupigania maisha ya mzazi ambaye alichelewa kufika kituoni waliweza kuokoa maisha ya mtoto na mama yasipotee akiwa kwenye huduma.

Dkt. Gwajima ametoa wito kwa wananchi kuhakikisha wanasikiliza ushauri wa wataalamu wa sekta ya Afya ili wawahi kufika kwenye vituo vya kutoa huduma kwa wakati hali itakayotoa fursa kwa wataalamu kuweza kutumia taaluma zao kuokoa maisha.

Amesema wizara ya Afya imeimarisha ufuatiliaji wake kwa msaada wa TEHAMA ili kufikia kila kituo cha kutoa huduma za Afya, hivyo wananchi wasiwe na wasiwasi na huduma zinazotolewa pia watoe ushirikiano wa taarifa kwa wakati ili kama kuna uzembe wowote ambao haujabainika uweze kuibuliwa na kuzuiwa.

Amesema, vifo vya wazazi na watoto wachanga havikubaliki na kwa kila kifo uchambuzi utafanyika mubashara ili kujiridhisha kuwa ilikuwa kinaepukika au hapana na kama juhudi zote stahiki zilifanyika kwa wakati ili mapitio ya vifo yataonyesha kuimarishwa ili kuweza kufikia vifo vyote nje ya vya uzazi na watoto wachanga.

Dkt. Gwajima ametoa wito kwa wananchi kutoa ushirikiano wao wa taarifa za kuridhika au kutoridhika kwa huduma kupitia namba za viongozi wa ngazi ya kituo, halmashauri, na mkoa zilizobandikwa kwenye mbao za matangazo ya kituo pia wanaweza kuwasilisha moja kwa moja wizarani kwenye namba 199 (namba ya kupiga) au 0734124191 namba ya Waziri wa Afya Dkt.Gwajima 0734124191 kwa kutuma ujumbe tu)

Kwa upande wake Dkt. Ahmad Makuwani, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya akina mama akiungana na mabingwa wengine kwenye kutoka hospitali mbalimbali za rufaa za mikoa na kanda pamoja na hospitali za halmashauri, vituo vya afya na zahanati amemuhakikishia Waziri kuwa ataratibu usimamizi endelevu wa mkakati huu ambao umeonesha kuwa na tija kwa ajili ya kuhakikisha zoezi hili ni ndelevu na lenye tija kwenye kuleta mshikamano wa kitaaluma wa kuboresha uwajibikaji kwenye utoaji huduma na kupunguza au kuondoa kabisa vifo hasa vile ambavyo vinaepukika.

Kikao hicho kilichoanza tangu tarehe 20/12/2021 kitakuwa kinafanyika kila siku na kuongozwa na wataalamu wabobezi kwa lengo la kufikia kila kituo ambako kifo kimetokea na kufanya uchambuzi wenye kuibua mazuri, mapungufu na kuelimisha sambamba na kuchukua hatua stahiki iwapo itabainika kuna uzembe.


from MPEKUZI

Comments