Taarifa Ya Jeshi La Polisi Mkoa Wa Mwanza


 TUKIO LA KWANZA; – WIZI WA MTOTO.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza tarehe 23.12.2021 lilifanikiwa kumkamata mwanamke mmoja aliyefahamika kwa jina la Rose Joshua @ Dinda, Miaka 27, Mkazi wa Buhongwa, kwa kosa la Wizi wa Mtoto jina linahifadhiwa Jinsia ya Kiume,mwenye umri wa miezi miwili, kitendo ambacho ni kosa kisheria.

Tukio hili limetokea tarehe 19.12.2021 majira ya 20:00hrs huko maeneo ya Dampo Soko la Machinga, kata ya Buhongwa, Wilayani Nyamagana, hii ni baada ya Mtuhumiwa kutengeneza mazoea ya karibu na Mama wa Mtoto aitwaye Stella Damas, miaka 22, mfanyabiashara mdogomdogo wa maeneo ya dampo soko la machinga-Buhongwa, ndipo baadae mtuhumiwa alimuomba Mama wa mtoto amsaidie kumbeba mtoto wakati akiendelea na shughuli zake za biashara kisha kutoweka na mtoto kusikojulikana.

Baada ya kitendo hicho, Mama wa mtoto alitoa taarifa Polisi ndipo ufuatiliaji wa haraka ulifanyika kwa kushirikiana na Polisi Mkoa wa Kigoma na baadae mtuhumiwa alikamatwa Mkoani Kigoma na kumuokoa mtoto akiwa hai na afya njema. Uchunguzi wa awali umebaini mtuhumiwa alifanya uhalifu huo ili kunusuru ndoa yake baada ya kukosa mtoto kwa muda mrefu.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linatoa wito kwa wazazi/walezi kuacha tabia ya kuwa na mazoea na watu wasiowafahamu ili kuepusha uhalifu wa aina kama hii. Pia linaendelea kuwasihi wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Jeshi lao ili liendelee kudhibiti uhalifu na wahalifu katika maeneo yote.

TUKIO LA PILI; – SHUKRANI ZA KRISMASI NA KUELEKEA MWAKA MPYA.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linawashukuru wananchi wote wa Jiji na Mkoa wa Mwanza kwa kusheherekea sikukuu za Krismasin na Boxing Day (siku ya kupeana zawadi) katika hali ya utulivu na amani, kwani kwa kipindi chote hicho kwa ujumla hali ilikua shwari wananchi walikwenda kwenye Mkesha na Ibada ya Krismas bila kupata tukio lolote la kihalifu, makanisa yote yalipewa ulinzi. Pia watoto walikwenda kwenye michezo bila bughudha zozote na wale waliokua kwenye starehe walisheherekea sikukuu vizuri bila kupatwa na tukio la kihalifu.

Kwa upande wa barabarani kwa ujumla Mkoa wetu haujaripotiwa tukio lolote la ajali za barabarani. Aidha Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linawashukuru wananchi wote kwa ushirikiano mkubwa waliotoa kwani pale palipokua na viashiri vya uhalifu walitoa taarifa na Polisi walifanya ufuatiliaji wa haraka, hivyo linawapa wananchi wote hongera sana.

Aidha katika kuelekea sikukuu ya Mwaka Mpya Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linaendelea kutoa wito kwa wananchi kusheherekea sikukuu ya Mwaka Mpya kwa amani na utulivu katika maeneo yao na kuwasihi wasije wakajihusisha na vitendo vya kiuhalifu na kwa yeyote atakayethubutu atashughulikiwa kwa mujibu wa sheria.

Sambamba na hilo Askari wataendelea kuimarisha ulinzi na usalama katika maeneo yote ya Jiji na Mkoa wa Mwanza kwa kufanya doria za miguu, magari, pikipiki na mbwa. Pia kwenye fukwe askari wa kikosi cha Polisi wanamaji wataendelea kufanya doria maeneo yote na kutoa elimu ya ulinzi shirikishi, halikadhalika askari wa usalama barabarani wataendelea kupangwa maeneo muhimu na kuhakikisha ajali hazitokei.

Hata hivyo ni marufuku wananchi kuchoma matairi barabarani, kurusha mawe na ni marufuku kupiga fataki bila kibali na kwa yeyote anayetaka kupiga fataki aombe kibali kwa Mkuu wa Polisi Wilaya husika (OCD) na kwa yeyote atakaekwenda kinyume na hivyo hatua stahiki za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linawatakia wananchi wote Heri ya Mwaka Mpya.


from MPEKUZI

Comments