Serikali kuzindua awamu ya pili ya kampeni ya kukabiliana na UVIKO-19


Serikali inatarajia kuzindua kampeni ya utekelezaji wa Mpango Shirikishi na Harakishi awamu ya Pili dhidi ya UVIKO-19 nchini Tanzania inayolenga kushirikiana wananchi na Wadau wa Maendeleo ili kuongeza chachu kwa watoa huduma ngazi ya Jamii kuelimisha na kuhamasisha wananchi kuchukua tahadhari na kupata chanjo.

Akizungumza  Desemba 19,2021 jijini Dodoma na waandishi wa habari , Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Prof. Abel Makubi, amesema uzinduzi huo utafanyika Desemba 22, mwaka huu jijini Arusha.

“Mtakumbuka kuwa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliridhia matumizi ya Chanjo ya UVIKO-19 na mnamo tarehe 23 Julai, 2021, kwa mara ya kwanza Tanzania ilianza kutoa chanjo hizi za UVIKO-19 kwa kuanza na chanjo ya Jenssen, baadae Sinopharm na Pfizer. Aidha, hadi jana Desemba 18, jumla ya wananchi 1,275,795 sawa na 2.21% walikuwa wamepata chanjo kamili na kupata kinga kamili dhidi ya UVIKO 19, lengo la serikali ni kufikia 60% ya wananchi wote,”

“Ili kufanikisha malengo ya awamu ya pili na matumizi ya watoa huduma ngazi ya jamii, Wizara na OR-TAMISEMI imeandaa Mwongozo wa Wawezeshaji wa Wahudumu wa Afya ya Jamii ikiwa ni pamoja na kuwatambua Wahudumu waliopo katika ngazi ya Vijiji, Mitaa na Vitongoji na kuanza kuwajengea uwezo kwa kuwapatia mafunzo kuhusu kinga ya UVIKO – 19 na umuhimu wa wananchi kuchanja.” amesema Prof. Makubi.

Amesema katika mikoa ya Mwanza, Dodoma, Manyara, Arusha, Dar es Salaam, Mbeya, Songwe, Kilimanjaro, Geita, Ruvuma na Morogoro tayari wahudumu zaidi ya 8,130 wamepatiwa mafunzo na wanaendelea na kazi ya uhamasishaji huku zoezi hili likiwa ni endelevu katika maeneo mengine nchi nzima.





from MPEKUZI

Comments