Serikali Kuja Na Mkakati Kukabiliana Na Vifo Vitokanavyo Na Uzembe Wa Baadhi Wa Wataalam Wa Afya.


 Na Atley Kuni, WAMJW- DODOMA.
Katika hali ya kuendelea kupunguza Vifo vya Mama na Mtoto,  Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima, amesema kuanzia sasa kutakuwa na Utaratibu wa Mikutano kwa Njia ya Mtandao (Zoom), kila siku baina ya wataalam wa Wizara, Mkoa na Kituo kilipo tokea kifo husika, ili kubaini endapo kuna uzembe uliojitokeza katika kumhudumia mzazi au mjamzito hadi akapoteza uhai.

Dkt. Gwajima amesema, lengo la kufanya hivyo ni kutaka kubaini endapo kuna uzembe au huduma ilienda sawa hatua zote, na kama ikibainika mtoa huduma kafanya uzembe basi kitakachofuata ni mhusika au wahusika kufikishwa kwenye  Mabaraza ya kitaaluma yanayosimamia taaluma husika.

Dkt. Gwajima, amesema zoezi hilo litakaloanza tarehe 20 Desemba, 2021, ni sehemu ya Mpango Mkakati wa Tano wa Sekta ya Afya uliozinduliwa Julai, 2021 ili kumsaidia mama awe na uzazi salama.

” Mimi naamini, vifo vingi vinazuilika na ukichunguza kwa undani utaona kuwa siyo vyote ni majaliwa ya Mungu bali vingine ni uzembe au kutojali kwa baadhi ya watoa huduma ambao wameshindwa kusimamia taaluma kwa misingi inayoongoza taaluma zao, hivyo kuanzia sasa tunaunda timu ngazi ya Wizara, ili kufanya Tathmini ya vifo vyote vinavyotokana na uzazi”. Amesema Dkt. Gwajima.

Katika hatua nyingine, Dkt. Gwajima, amepata fursa ya kuzungumza na Madaktari Wanafunzi waliopo Katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma,  ambapo katika mazungumzo yao amewataka Madaktari hao, kuishi miiko inayo ongoza taaluma yao.

Awali alipokea changamoto mbalimbali za Madaktari hao wanafunzi, ambapo walipendekeza Matumizi ya Teknolojia katika uendeshaji wa shughuli za Hospitali katika wakati wa sasa.

“Mhe. Suala la kutumia Makatarasi linazorotesha sana ufanisi na kupoteza muda mwingi, laiti kama data zingekuwa zinachakatwa kidijitali kazi yetu ingekuwa rahisi sana.” amenukuliwa mmoja wa Madaktari wanafunzi hao.

Hata hivyo, Mhe. Waziri, aliahidi kulifanyia kazi suala hilo. Pamoja na mapendekezo mengine yote waliyo wasilisha kwa njia ya kuandika na yale atakayo pokea kupitia simu ya kiganjani ambapo aliwapa namba ya kuwasiliana.

Dkt. Gwajima anafanya ziara katika Hospitali hiyo ikiwa ni mwendelezo wa Ziara zake katika kukagua shughuli za Afya.




from MPEKUZI

Comments