Rais Samia: Tutakopa fedha kujenga Reli ya Kisasa (SGR)


Rais wa Tanzania, Samia amesema ni lazima serikali ikope ili kumaliza mradi wa Reli ya Kisasa (SGR).

Rais Samia ameyasema hayo leo Desemba 28, 2021 katika hafla ya utiaji saini mkataba wa ujenzi wa SGR kipande cha tatu kutoka Makutupora hadi Tabora chenye urefu wa kilometa 368, kitakachogharimu dola za Kimarekani 1.908 bilioni sawa na Sh4.41 trilioni kati ya Shirika la Reli Tanzania (TRC) na Yapi Merkez kutoka Uturuki.

Amesema uwekezaji huo ni wa Sh14.7 trilioni hivyo usipoendelea itakuwa ni upotevu wa fedha zilizotumika awali, hivyo ni lazima kukopa ili kuuendeleza.

“Kwa sababu fedha hizi hatutazitoa kwenye tozo wala hatutazitoa kwenye kodi tunazokusanya ndani, ni lazima tutakopa kwa hiyo tutakopa ili kukamirisha mradi huu kwa sababu tusipokamilisha fedha tulizoilaza pale ndani itakuwa haina kazi na haina maana kwahiyo ni lazima tumalize huu mradi, tukope tumalize mradi,” amesema Rais Samia.

Amesema mradi wa SGR ulianza kutekelezwa kwa mujibu wa ilani ya CCM ambapo ujenzi wa awamu ya kwanza kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza ulianza mwaka 2017 na umegawanyika katika vipande vitano ukipita katika mikoa tisa.

Ameendelea kusema kuwa ujenzi huo unaendelea katika vipande vitatu cha Dar es Salaam- Morogoro (asilimia 95), Morogoro- Makutupora (asilimia 77) na Mwanza-Isaka (asilimia4), ambapo ni jumla ya kilometa 1063 za njia kuu za reli pamoja na njia za kupishana.

“Hii ni kazi kubwa yenye kuhitaji uthubutu mkubwa wa serikali na wananchi wake. Hii inafanya uwekezaji wa ujenzi wa vipande vinne kati ya vitano vinavyoendelea kufikia kiasi cha Sh14.7 trilioni ukijumlisha na kodi,” amesema.

Ameongeza kuwa tayari ameshaagiza Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kupitia TRC kukamilisha taratibu za manunuzi kwa ajili ya kumpata mkandarasi wa ujenzi kipande kilichobaki cha Tabora – Isaka na kipande kipya cha awamu ya pili kutoka Tabora hadi Kigoma.


from MPEKUZI

Comments