Dkt Biteko Aagiza Kusimamishwa Kazi Maafisa Saba Wa Ofisi Za Madini Mikoa Kanda Ya Ziwa


Na. Mwandishi wetu, Kahama
Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko amemuagiza Kaimu Mtendaji wa Tume ya Madini Mhandisi Yahya Samamba, kuwasimamisha kazi Maafisa saba wa Ofisi za Madini za Mikoa ya Kanda ya Ziwa kutokana na kutokuwa waaminifu katika shughuli zao za usimamizi wa Sekta ya Madini .

Agizo hilo amelitoa Wilayani Kahama Mkoa wa Shinyanga alipokutana na Wafanyabiashara wa Madini wa Kanda ya Ziwa kwa lengo la kusikiliza kero mbalimbali zinazowakabili wafanyabiashara hao.

Dkt, Doto Biteko amesema, kuna baadhi ya watumishi wa Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa ambao sio waaminifu na wanajihusisha na udanganyifu kwenye biashara ya madini ikiwemo kuwapunguzia wachimbaji viwango vya ubora wa madini yao ili wajipatie fedha.

“Nichukue fursa hii kuwatadharisha Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa yote nchini kuhakikisha mnawafuatilia kwa karibu Maafisa wenu wanaoshirikiana na baadhi ya wafanyabiashara ambao wamekuwa wakiwaibia wachimbaji wadogo wa madini kwa kupaka mafuta kwenye mashine ya kupimia ubora wa dhahabu na kusababisha kupata kiwango cha chini cha ubora wa madini ukilinganisha na uhalisia wa madini yenyewe,” amesema Dkt. Biteko.

Aidha, Dkt. Biteko amesema, kumeibuka kwa kundi la baadhi ya wafanyabiashara wa madini ya dhahabu wanaojihusisha na vitendo vya kuwatapeli wafanyabiashara wa nje ya nchi kwa kuwaomba fedha ili wawanunulie madini lakini wanashindwa kufanya hivyo na kujificha kwenye kisingizio kuwa wanaumwa Uviko-19 baada ya kupewa fedha.

Dkt. Biteko amesema kuwa, kundi hilo limekuwa likipokea fedha za ununuzi wa madini kutoka kwa wafanyabiashara wa nje ya nchi na kupiga picha maboksi ya madini yaliyofungwa siri za Wizara ya Madini ambazo ni feki na kuwatumia kwa njia ya mitandao kuwa mzigo uko njiani, jambo ambalo sio kweli na wanapotumiwa fedha wanazima simu zao.

“Hivi karibu amekuja mzungu ofisini kwangu analia kutapeliwa dola za Kimarekani 800,000 sawa na kiasi cha shilingi bilioni 7.2, tulipompigia simu mhusika aliyepatiwa fedha hizo alirusha maneno na kusingizia kuwa anaumwa ugonjwa wa korona jambo ambalo sio kweli," amesema Dkt, Biteko.

Pia, Dkt. amesema, hapo awali wafanyabiashara wa madini walikuwa wakituhumiwa katika shughuli ya utoroshaji wa madini na kusababisha serikali kukosa maduhuri lakini baada ya kulidhibiti jambo hilo kwa sasa wameibuka katika kuwatapeli wafanyabiasha fedha zao kwa madai ya kuwanunulia madini.

Sambamba na hayo, Dkt. Biteko amesema, kuna baadhi ya Masoko ya Madini yamekuwa yakifanya vema katika ukusanyaji wa maduhuri ya serikali ambapo Mwaka 2020/2021 Soko la Madini la Mkoa wa Geita liliongoza nchi nzima kwa kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 211.5, soko la pili ni Soko la Mkoa wa Mara ambalo lilikusanya kiasi cha shilingi bilioni 109.3 ikifuatiwa na Soko la Madini Mkoa wa Kimadini la Kahama ambalo lilikusanya kiasi cha shilingi bilioni 93.7.

Awali, Waziri Biteko alikutana na Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa Kumi na moja ya Kimadini ikiwemo Kahama, Mbogwe, Geita, Shinyanga, Mara, Simiyu, Mwanza, Singida, Kigoma, Kagera na Tabora ambapo aliwataka kuwa waaminifu katika shughuli zao baada ya kubaini mapungufu katika baadhi ya Mikoa hasa katika masuala ya usimamizi, ufuatiliaji na uaminifu.


from MPEKUZI

Comments