Serikali Yadhamiria Kumaliza Migogoro Ya Ardhi Nchini


 Na Mwandishi Wetu, MWANZA
Serikali ya awamu ya sita chini Rais Samia Suluhu Hasan imedhamiria kumaliza kero na migogoro ya ardhi nchini kwa kutatua iliyopo na kuweka mikakati ya kuzuia migogoro mipya ikiwemo utwaaji maeneo ya wananchi bila kulipa fidia

Hayo yalisemwa na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula mwishoni mwa jijini Mwanza wakati wa kutatua migogoro ya muda mrefu ya ardhi iliyopo wilaya ya Nyamagana ukiwemo mgogoro wa wananchi na Mwekezaji kampuni ya Pamba Engineering uliopo kata ya Mhandu.

Mgogoro mwingine ni baina ya Msimamizi wa Mirathi Ndugu Abuu mwana familia ya Marehemu Mzee Seif eneo la Miembeni mtaa wa Nera kata ya Isamilo kuhusu umilikishwaji eneo lao la urithi na ulipwaji fidia kwa wananchi wa mtaa wa Kisoko kata ya Luchelele kutokana na Serikali kutwaa eneo lao kwa ajili ya ujenzi wa shule

Katika kutatua mgogoro kati ya wananchi na Mwekezaji Pamba Engineering Naibu Waziri Dkt Mabula ameelekeza wananchi kumilikishwa eneo linalolalamikiwa kati yao na Mwekezaji katika Kata ya Mhandu kufuatia wananchi hao kukidhi matakwa yote ya kisheria na kulipa gharama za umilikishaji huku Familia ya Marehemu Mzee Seif ikielekezwa kupatiwa viwanja Saba vilivyopatikana baada ya kupimwa eneo lao la asili alilolinunua marehemu baba yao miaka ya themanini kwa aliyeteuliwa kusimamia mirathi baada ya kujiridhisha

Kuhusu eneo la mtaa wa Kisoko kata ya Luchelele Mhe Dkt Mabula mbali na kuwataka wananchi wa mtaa huo kushirikisha viongozi waliopo katika maeneo yao kutatua kero mbalimbali za ardhi alimtaka Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza Sekiete Yahaya kuhakikisha anawalipa fidia wananchi wote 20 waliotwaliwa maeneo yao na Serikali kwa ajili ya ujenzi wa shule mapema kabla ya mwaka wa fedha 2021/2022 kuisha ambapo kiasi cha shilingi milioni 350 zinadaiwa na wananchi hao

‘’Nikuombe Mkurugenzi wananchi hawa wamekaa muda mrefu wakisubiri fidia wengine wameshindwa hata kuendeleza maeneo yao  kwa sababu hawajalipwa  fidia, naomba wananchi hawa walipwe wote kabla ya mwaka wa fedha wa sasa kuisha ‘’ Alisema Dkt Mabula

Kwa upande wake mkurugenzi wa jiji la Mwanza Sekiete Yahaya alisema kuwa,  maeneo yanayotwaliwa kwa ajili ya taasisi za Serikali kama shule na huduma nyengine yatalipwa fidia kwa awamu mpaka deni lote litakapokwisha.

 ‘’Mhe Naibu Waziri naahidi kulipa fidia kwa awamu kuanzia kipindi hiki cha kati kati ya mwaka wa fedha 2021/2022 na kumaliza jumla ya milioni 150 kufikia mwishoni mwaka huu wa fedha’’ alisema Yahaya.

Naye Diwani wa kata ya Luchelele Vicent Lusana alifafanua kuwa wanafunzi wanaotoka eneo lake wamekuwa wakitembea umbali mrefu kwa ajili ya kufuata elimu na kusisitiza kuwa ipo haja kwa Serikali kuharakisha ulipwaji wa fidia ili waanze ujenzi wa shule kwa lengo la kuwafanya  wanafunzi wa eneo hilo kupata elimu katika umbali mfupi na kuwaepusha na changamoto mbalimbali ikiwemo mimba za utotoni

Akihitimisha Kamishina wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Mwanza Elia Kamihanda ametaka kuzingatiwa utengwaji maeneo kwa ajili ya shughuli za Umma katika zoezi la upimaji na upangaji wa mji huku akiwaasa wananchi kuhakikisha wanayalinda maeneo yote yanayotengwa kwa matumizi ya jamii ikiwemo malalo na maeneo ya wazi.


from MPEKUZI

Comments