Na. Beatrice Sanga- Maelezo
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Geofrey Mwambe amebainisha kuwa Serikali itaendelea kuiunga mkono Sekta binafsi kwa kuweka mazingira wezeshi katika kuhakikisha sekta binafsi inashiriki ipasavyo katika kukuza uchumi wa nchi na kujenga uchumi jumuishi ili kuchochea uchumi na kukuza ajira na kipato kwa wananchi.
Ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa mkutano wenye lengo la kuwaleta pamoja wadau mbalimbali wa sekta binafsi ili kutoa hamasa kwa sekta hiyo kushiriki ipasavyo katika Utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko-19 uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es salaam.
Katika hotuba yake Waziri Mwambe amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa, Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha upatikanaji wa mkopo wenye masharti nafuu wa thamani ya Shilingi Trilioni 1.3 kwa ajiri ya kukabiliana na athari za Uviko -19 ambapo fedha hizo zimelenga kuleta ustawi katika sekta mbalimbali za huduma ikiwemo elimu, afya, maji na utalii.
“Naomba nitumie fursa hii, kutoa shukrani za dhati kwa Mheshimiwa, Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa dhamira yake kubwa aliyoionesha katika mapambano dhidi ya Uviko-19 kwa kuwezesha upatikanaji wa Shilingi Trilioni 1.3 ambazo ni mkopo wenye masharti nafuu kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF) ili kutekeleza Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko-19”, Amesema Mwambe
Mwambe ameeleza kuwa, utekelezaji huu, utahusisha manunuzi ya bidhaa na huduma mbalimbali hivyo sekta binafsi itahitajika kushiriki ipasavyo ambapo bidhaa na huduma zinazohitajika ni pamoja na vifaa vya ujenzi, mashine na vifaa mbalimbali vya hospitali, elimu na maji, ujenzi na ukarabati wa majengo ya shule, vyoo na hospitali, ujenzi wa maeneo ya kufanyia bishara kwa ajili ya wanawake, vijana na wenye ulemavu pamoja na ujenzi na ukarabati wa mtandao wa barabara katika hifadhi za wanyama na ukarabati wa maeneo ya urithi na kutoa vivutio kwa wawekezaji katika tasnia ya utalii.
Ameongeza kuwa Utekeelezaji wa miradi hiyo utachangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa sekta binafsi nchini kwa kushiriki ipasavyo katika utekelezaji wa mpango hivyo ni wakati muafaka kwa sekta binafsi kujipanga kuhakikisha inatumia fursa hiyo kushiriki katika utekelezaji wa mpango na kuchangia katika kufanikisha jitihada za serikali za kukuza uchumi na kuzitaka sekta binafsi kudhalisha bidhaa na kutoa huduma zenye ubora na viwango vinavyohitajika na soko.
“nichukue fursa hii kuwaomba na kuwakumbusha sekta binafsi kuhakikisha inatekeleza wajibu wake kwa kufanya kazi zenye viwango kulinganana na mahitaji ya soko na uzalishaji wa bidhaa zenye kukidhi viwango vinavyohitajika na kutosheleza na kukidhi mahitaji ya utekelezaji wa mpango, hatua hii itawezesha bidhaa na huduma zinazotolewa na watanzania kuwa shindani katika bei na ubora wa bidhaa” Amesema mwambe
Utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO 19 ulizinduliwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 10 Oktoba, 2021 Jijini Dodoma, Ambapo shilingi trilioni 1.3 zilizotolewa na Shirika la Fedha Duniani (IMF) zimelenga kuleta ustawishaji katika sekta za huduma ikiwemo Elimu, Afya, Maji na Utalii.
Kati ya fedha hizo, TZS bilioni 139.4 zinaenda kutekeleza miradi katika sekta ya maji; TZS bilioni 466.9 zinaenda sekta ya elimu; TZS bilioni 64.9 zinaenda Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia; TZS bilioni 302.7 zinaenda Ofisi ya Rais-TAMISEMI; TZS bilioni 5.0 zinaenda kwa ajili ya uwezeshaji wananwake, vijana na wenye ulemavu; TZS bilioni 5.5 zinaenda kwa kaya maskini; TZS bilioni 90.2 zinaenda sekta ya utalii; TZS bilioni 231.0 zinaenda Zanzibar; na TZS bilioni 5.0 zitatumika katika kuratibu zoezi hili.
Mwisho
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment