Rais Wa Burundi Asifu Uongozi Wa Rais Samia


Na Ahmed Sagaff – MAELEZO
Rais wa Jamhuri ya Burundi, Mhe. Evariste Ndayishimiye amesifu uongozi wa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Rais Ndayishimiye ametoa sifa hizo jana  jijini Dodoma wakati akizindua kiwanda cha mbolea cha Itracom kilichojengwa na muwekezaji kutoka Burundi.

“Rais Samia anaweka utawala bora, anaongoza vizuri, anawaunganisha Watanzania na watu wa Burundi,” ameeleza Mhe. Ndayishimiye.

Awali akizungumza kwenye mkutano wa waandishi wa habari uliofanyika Ikulu ya Chamwino jijini humo, Rais Ndayishimiye amempongeza Rais Samia kwa kuwa kiongozi wa kike anayeonesha mfano mzuri barani Afrika na ulimwenguni kote.

“Nimekuja kukupongeza kwa mfano mzuri wa uongozi unaouonesha Afrika na duniani kama mwanamke,” amebainisha kiongozi huyo.

Sambamba na hilo, Mhe. Ndayishimiye ameipongeza Tanzania kwa kujitolea katika kutimiza malengo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

“Naipongeza Tanzania kwa juhudi zake inavyoimarisha Jumuiya ya Afrika Mashariki na inavyojitolea kutimiza malengo ya jumuiya hiyo,” amepongeza Rais Ndayishimiye.

Pamoja na hilo, Rais Ndayishimiye ameishukuru Tanzania kwa kuwapokea na kuwahifadhi wakimbizi kutoka Burundi tangu uongozi wa Hayati Julius Kambarage Nyerere.

“Zaidi ya wakimbizi 200,000 kutoka Burundi walipewa uraia na Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, sasa wana hadhi kama raia wa Tanzania,” amedokeza.

Aidha, Rais huyo amewashukuru marais wa awamu zote wa Tanzania kwa jitihada za kurejesha amani nchini Burundi.


from MPEKUZI

Comments