Rais Samia Aipongeza Wizara Ya Utamaduni, Sanaa Na Michezo Kwa Ubinifu


Na. John Mapepele, WSUM
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mhe, Samia Suluhu Hassan ameipongeza  Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa ubunifu wa kuandaa mikakati mbalimbali ya kuendeleza sekta za Sanaa, Utamaduni na Michezo ikiwa ni pamoja na kuandaa Tamasha kubwa la Kimataifa la Sanaa na Utamaduni Bagamoyo linaoanza kesho oktoba 28 hadi 30  mjini Bagamoyo.

Rais Samia ameyasema hayo Oktoba 27, 2021 Ikulu  jijini Dar es Salaam kwenye  hafla maalum aliyoiandaa kwa ajili ya  kuipongeza Timu ya Taifa ya Soka  ya Wanawake (Twiga Stars) kwa kutwa Kombe la COSAFA hivi karibuni.

“Ili kufanikisha ushindi naomba nitambue TFF, Wizara na Wadau wengine hongereni kwa umoja wenu, najisikia  fahari Twiga Stars  kushinda ugenini na kuleta  kombe  nyumbani” amefafanua Mhe. Rais

Tamasha la kimataifa la Sanaa na Utamaduni Bagamoyo lenye kauli mbiu isemayo “Sanaa ni Ajira” lina lengo la kukuza na kuendeleza sanaa na utamaduni wa mtanzania pia kukutanisha  watu wa tamaduni tofauti kutoka  sehemu mbalimbali duniani ili kuonyesha utajiri wao wa  sanaa na utamaduni.

Rais Samia pia amepongeza ubunifu na uratibu uliofanywa wa kuandaa Tamasha la Michezo kwa Wanawake la Tanzanite  lililofanyika hivi karibuni  jijini Dares Salaam.

Amesema wakati akikabidhiwa uchifu hivi karibuni na Umoja wa Machifu nchini  mkoani Mwanza aliiagiza Wizara  kuwa na Tamasha  la Uchifu ambalo litakuwa likizunguka kila mkoa  na kuwataka machifu washirikishwe kikamilifu ili kukuza utamaduni  ndani ya nchi yetu.

Ameongeza kuwa mafanikio makubwa yaliyopatika kwenye sekta za Sanaa, Utamaduni na Michezo katika kipindi hiki ni kutokana na uwekezaji uliofanywa na Serikali ambapo amesema Serikali ilitenga 1.5 bilioni na kiasi kingine   kimetoka kwenye  michezo ya  kubashiri.

Ameipongeza Wizara kwa kuratibu Tamasha kubwa la Bara la Afrika la warembo, mitindo na watanashati ambalo  limetoa  washindi sita kwenda kwenye  mashindano hayo kidunia nchini Brazil Aprili 2022 na kuitaka Wizara  ianze  maandalizi kwa ajili ya washiriki hao mapema ili waende wakiwa  wanajiamini.

Mhe. Rais ametumia tukio hilo kuzipongeza Timu za Kriketi za wanaume na wanawake zilizoshika nafasi ya tatu katika shindano la Bara la Afrika na  kuitaka Wizara kuupa kipaumbele mchezo huo ili uweze kufika kwenye ngazi ya kimataifa.

Pia ameipongeza Timu ya Soka ya Wanawake ya Taifa chini ya umri wa miaka 20 kwa kuendelea  kufanya vizuri kwenye  mashindano  ya kuelekea kombe la dunia na kusisitiza kuwa  yeye kama Rais yupo bega kwa bega  na timu hiyo ambapo ameitaka Wizara  kuwaibua  makocha wengine wa kike na kiume  na kuwapatia mafunzo ili wawe wa kimataifa watakaosaidia kuinua kiwango cha soka nchini.

Amesema  kutokana na kufanya vizuri kwenye  michezo, mataifa  makubwa  duniani  yameanza  kufuatilia  wachezaji nchini.

“Macho ya Timu kubwa wanafuatilia dumisheni nidhamu” amesisitiza  Mhe Rais

Kwa upande mwingine Mhe. Rais amesema anatambua  taasisi za Wizara kama BASATA, COSOTA na Bodi ya Filamu zina bajeti  ndogo ambapo amesema baada ya miezi  sita zitakwenda kupitiwa na kuelekeza Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kukaa na Wizara ya Fedha kupeleka hoja  na amesisitiza  kuwa atasaidia  suala hili ili zipatiwe bajeti ya kutosha ziweze kufanya vizuri.

“Naomba Wizara mkae na Wizara ya Fedha mjieleze vizuri nami nitaweka  nguvu huko”. Amefafanua Mhe.Rais Samia

Ameitaka Wizara kuwa  wabunifu na kuvutia vijana  katika  michezo  ili kuwandaa kwenye ajira ambapo ameagiza kupata mrejesho wa suala hili katika miezi mitatu ijayo.

Ameitaka  pia Wizara kuangalia na kujadili vyanzo  vipya vya fedha kufadhili Sanaa, Utamaduni na Michezo ambapo ametaka kuangalia  maeneo  ya kuwapunguzia tozo na kodi wasanii na wanamichezo pia kuwapa vivutio vya kikodi ili wawekezaji waweze kuwekeza kwenye maeneo hayo.

Kwa upande mwingine ameitaka Wizara  kuja na  mpango madhubuti wa kufadhili mchezo wa soka kwa wanaume na wanawake  na ameitaka  Wizara ya Utamaduni kushirikiana na TAMISEMI kuibua  vipaji  katika michezo ya UMISSETA na UMITASHUMTA na kuvikuza.

Amefafanua kuwa wanamichezo wana nafasi kubwa  ya kutambulisha utalii wa nchi yetu duniani.

Akizungumzia kuhusu Muundo wa Wizara amesema  amefanya mabadiliko ya Wizara kwa kuiondoa Idara  ya Habari kuipeleka mahali inakohusika ili  viongozi wa Wizara  wajielekeze zaidi kwenye sekta za Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Amewapongeza  Mawaziri kwa  kuaminiwa na kuendelea kutumikia kwenye nafasi zao na kuwataka kwenda kushirikiana na kuchapa kazi siyo kugombana.

Ameeleza kuwa sekta za utamaduni, Sanaa na Michezo ni  sekta za kipaombele ambazo pia zimeainishwa kwenye Ilani ya Uchaguzi 2020-2025 na zinatoa ajira kwa wananchi.





from MPEKUZI

Comments