Mwanasheria wa kampuni ya Kufua Umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL), Joseph Makandege, ameiomba tena kufanya mazungumzo na ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) ili akiri makosa yanayomkabili na kwenda kumzika baba yake.
Mshtakiwa huyo anakabiliwa na mashtaka matano likiwemo la kuisababishia serikali hasara ya dola za Marekani 980,000 na kutakatisha fedha.
Mwakandege ameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ipange siku ya Ijumaa kwa ajili ya suala hilo kwa kuwa watakuwa wamekamilisha utaratibu wa kufanya mazungumzo na DPP.
Awali, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Ladislaus Komanya aliiambia mahakama wametaarifiwa kuwa mshtakiwa huyo anataka kufanya mazungumzo na DPP ili aweze kukiri makosa yanayomkabili.
Komanya alidai kumbukumbu zao zinaonesha mshtakiwa huyo aliwahi kueleza nia ya kufanya mazungumzo na DPP lakini alijiondoa.
Baada ya maelezo hayo, wakili wa mshtakiwa huyo, Alex Balomi alidai ni kweli mshtakiwia huyo ana nia ya kufanya majadiliano na DPP kama alivyoomba katika barua yake ya awali.
Baada ya maombi hayo Komanya alisema: “Sisi tupo tayari kufanya naye mazungumzo hata leo au kesho, hivyo hakuna shida yeyote siku ya Ijumaa tunaweza kukamilisha ili tuweze kumsaidia mshtakiwa aweze kwenda kuzika.”
Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi, alikubaliana na maombi ya pande zote mbili kabla ya kuliahirisha shauri hilo hadi Oktoba 22,2021.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment