WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan imetenga shilingi bilioni 170 kwa ajili ya ujenzi wa Mkongo wa Taifa katika mwaka wa fedha 2021/2022.
“Lengo letu ni kuwawezesha watoa huduma za mawasiliano kutumia miundombinu hii kuboresha huduma za mawasiliano nchini na kurahisisha ufikishwaji wa intaneti kwenye ofisi mbalimbali za sekta ya umma na binafsi”
Ameyasema hayo jana (Ijumaa, Oktoba 22, 2021) wakati alipofungua Mkutano wa Tano wa Mwaka wa TEHAMA Tanzania uliofanyika katika katika ukumbi wa mikutano wa AICC, jijini Arusha. Amesema fedha hizo zitawezesha kujenga kilomita 4,244 za Mkongo ili kufikisha jumla ya kilomita 12,563.
Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kuiagiza Wizara ya Habari, Sayansi na Teknolojia ya Habari isimamie kwa karibu mradi wa upanuzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ili wananchi wengi zaidi washiriki katika ujenzi wa uchumi wa kidijitali.
“Hivi sasa Serikali imejenga kilomita 8,319 za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano hadi mwezi Septemba 2021. Malengo yetu kama Serikali ni kujenga hadi kilomita 15,000 ifikapo mwaka 2024/2025. Hili linahitaji uwekezaji mkubwa na Serikali imejipanga kuwekeza vilivyo lakini pia tunakaribisha wabia na wawekezaji katika eneo hili pamoja na maeneo mengine ya TEHAMA.”
Amesema kuwa miundombinu ya TEHAMA ni uti wa mgongo wa maendeleo ya kidijitali, hivyo nchi inahitaji kuongeza idadi ya watumiaji wa intaneti kufikia zaidi ya asilimia 80 nchi nzima kutoka asilimia 45. “Serikali imejiwekea lengo la kuongeza mtandao wa urefu wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ili kufikisha huduma bora na zenye gharama nafuu kwa wananchi wote.”
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa katika kipindi cha miaka mitano ijayo Serikali imedhamiria kuipeleka Tanzania kwenye ramani ya Ulimwengu kama moja ya nchi ambayo TEHAMA imeleta mageuzi makubwa ya kiuchumi.
Pia, Waziri Mkuu ameiagiza Tume ya TEHAMA ihakikishe inaweka mikakati mahsusi ya kusajili wataalamu wa TEHAMA ili kufikia lengo la usajili wa wataalamu 5,000 ifikapo mwaka 2025.
“Wizara ya Habari, Sayansi na Teknolojia ya Habari pia ishirikiane na Sekta binafsi katika kuongeza ufanisi wa kiutendaji. Angalieni pia uwezekano wa kufanya kazi na makampuni makubwa yaliyobobea katika sekta hii ili kujenga uchumi wa kidijitali.”
Baada ya kufungua mkutano huo Mheshimiwa Majaliwa pia amezindua mwongozo wa usajili wa wataalamu wa TEHAMA na kutoa vyeti kwa baadhi ya wataalamu wa TEHAMA ambao wamesajiliwa.
Mhe. Majaliwa pia ameitaka Wizara ya habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari washirikiane na Eizara ya mambo ya ndani katika kuhakikisha wanaweka Kamera za Usalama katika miji ili kukabiliana na changamoto ya uhalifu
Naye, Waziri wa Habari, Sayansi na Teknolojia ya Habari Dkt. Ashatu Kijaji amesema wizara yao imejipanga kujenga kituo mahiri cha kukuza utaalamu na tafiti nchini ambacho kitajengwa jijini Dodoma kwa kupitia Mradi wa Tanzania ya Kidijitali “Digital Tanzania”.
Amesema Wizara yao itakuwa mstari wa mbele kwa upande wa masuala ya kidijitali kwa kuangalia na kushauri sheria, kanunina na taratibu hitajika ili ziweze kuchochea na kuvutia ubunifu wa bidhaa na huduma za kidijitali zenye tija kiuchumi na zinazozingatia maadili ya Taifa.
Pia, Dkt. Kijaji amesema katika kuchochea ujenzi wa Taifa la kidijitali, wamebuni utaratibu wa kutoa tuzo maalum kwa wizara, idara, halmashauri, taasisi, kampuni na wabunifu wanaofanya kazi nzuri na jamii ikanufaika na matunda ya kazi na ubunifu wao kupitia TEHAMA.
Miongoni mwa waliotunukiwa tuzo ni pamoja na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kulibeba suala la TEHAMA kwa nguvu zake zote na kuliweka kwenye vipaumbele vya Serikali ya awamu ya sita ambayo anaiongoza.
Amesema wizara yao inaamini kwa kupitia utaratibu huo utakaokuwa unafanyika kila mwaka utatoa ushawishi mkubwa hasa katika eneo la ubunifu na kuchochea matumizi ya kidijitali ili Tanzania iweze kuwa Taifa la kidijitali.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment