Samirah Yusuph,
Itilima. Maambukizi ya minyoo tumbo inayosababisha ugonjwa wa kichocho wilayani Itilima Mkoa wa Simiyu yamezidi kupanda kutoka asilimia 10 hadi kufikia asilimia 57 kwa mwaka huu 2021.
Taarifa hiyo imetolewa na mganga mkuu wa wilaya hiyo Anord Musiba alipokuwa katika uzinduzi wa zoezi la unyweshaji dawa za minyoo kwa watu wazima lililofanyika jana Octoba 27,2021 katika kata ya Budalabujiga wilayani hapo.
Musiba alisema kuwa wilaya hiyo imekuwa na idadi kubwa ya maambukizi katika kata 12 ambapo baadhi ya kata zinakiwango kikubwa cha maambukizi hadi kufikia zaidi ya asilimia 60.
"Dawa zinazotolewa ni kinga pia ni tiba ikiwa wananchi watabadili mtindo wa maisha kwa kufuata matumizi sahihi ya choo, kunawa mikono, kutumia maji safi na salama pamoja na kuepuka kuoga katika madimbwi".
Akielezea mkakati wa kupambana na maambukizi hayo mkuu wa wilaya ya Itilima, Faiza Salim alisema hatua ya unyweshaji dawa ni mwanzo wananchi wanawajibu wa kuhakikisha wanazingatia usafi katika maeneo yao pamoja kuhakikisha kila kaya inakuwa na choo ili kuzuia maambukizi.
Amesema bila kuzuia maambukizi katika ngazi ya chini zoezi la unyweshaji wa dawa litakuwa halina mafanikio kwa sababu bado matumizi ya choo ni madogo wananchi bado wanajisaidia vichakani.
"Hivyo watendaji wa vijiji lazima wahakikishe katika maeneo yao wananchi wanatumia vyoo na kila kaya inakuwa na choo ili kukabiliana na maambukizi haya"
Baadhi ya wananchi wa kata ya Budalabujiga walieleza kuwa zoezi hili limekuwa ni hamasa kwa wananchi ambao awali walikuwa na imani potofu ya kudhani kuwa dawa zinazotolewa zinamadhara kwa binadamu.
"Wengi hawatumii vyoo kwa sababu walizoea kwenda vichakani kwa sasa tunaendelea kuhamasisha wananchi wajenge vyoo na kuvitumia ili kupambana na kichocho" Alisema Masho Lukuba mwenyekiti wa kijiji cha Budalabujiga.
Meneja wa mradi wa kupambana na magonjwa yasiyopewa kipaumbele kutoka shirika lisilo la kiserikali world vision, Irene Abusheikh alisema wamejipanga kupunguza na kutokomeza kichocho.
"Zoezi litafanyika kwa watoto kuanzia miaka 5 hadi wazee lengo ni kuboresha na kudumisha ustawi wa familia na jamii kwa ujumla"
Zoezi la utoaji wa dawa za kichocho litafikia wananchi 136,000 wa wilaya ya Itilima katika kata 12 ambazo zimepewa kipaumbele kutokana na maambukizi ya kichocho kuwa katika kiwango cha juu.
Mwisho.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment