“Vyama Vya Wafanyakazi Vina Tija, Vitumieni Vyema” Waziri Mhagama


NA MWANDISHI WETU, DODOMA
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama amesema Vyama vya Wafanyakazi Nchini vina mchango mkubwa katika upatikanaji wa maendeleo ya Taifa.

Ameyasema hayo  Septemba 29, 2021 Jijini Dodoma katika Mkutano Mkuu wa Uchaguzi Taifa wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGHE) ambapo alisema Serikali inaendelea kutatua changamoto zinazowakabili wafanyakazi  na kuboresha miundombinu  ili watekeleze majukumu yao kwa weledi na uadilifu.

Alisema ni nia ya Serikali kuhakikisha inaondoa changamoto zilizopo kati ya mwajiri na mwajiriwa huku akihimiza uwepo wa mabaraza ya wafanyakazi mahala pa kazi kama sehemu ya kutafuta ufumbuzi pindi migogoro inapojitokeza kwa kufanya mazungumzo kama daraja la mahusiano mema.

“Ninaamini nia njema ya viongozi wetu hawa Rais Samia Suluhu Hassan, Mkamu wa Rais, Waziri Mkuu na sisi kama wasaidizi wao katika kuwathamini wafanyakazi wa sekta ya umma na binafasi kama mchango mkubwa wa ustawi wa maendeleo ya Taifa letu na niwaombe zile changamoto mnazoona ziko ndani ya uwezo wenu mzifanyie kazi haraka,”alisema Waziri Mhagama.

Pia amemuagiza Msajili wa  Vyama vya Wafanyakazi nchini kuweka utaratibu wa kuandaa mafunzo maalumu kwa Viongozi wa TUGHE kuimarisha chama chao na kutumia fursa hiyo kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi huku akisistiza kufuatwa kwa sheria  za uamisho wa viongozi wa wafanyakazi kufuatia baadhi ya watu kujichukulia uamuzi wa kuhamisha viongozi bila kufuata sheria kudhoofisha Chama.

Vilevile amewataka waajiri kuatambua umuhimu wa Vyama vya Wafanyakazi na Viongozi wa Vyama vya wafanyakazi katika maeneo yao kama daraja la kuwaunganisha waajiri na wafanyakazi kuondoa migogoro inayoweza kuepukika na kuheshimu Mabaraza mahala pa kazi.

“Ni kweli kuna baadhi yetu sisi viongozi  wa Vyama vya wafanyakazi tunakuwa chanzo cha migogoro badala ya kujenga amani sehemu za kazi  niwaase ili tuweze kwenda sawasawa kila mtu atimize wajibu wake ningetamani katika kipindi changu cha uongozi kuona  mahusiano ya wafanyakazi na waajiri yanakuwa ya hali ya juu,”alieleza .

Hata hivyo alibainsiha kwamba Serikali itaendelea kufanya marejeo ya sheria za utatuzi wa migogoro kwa kulingalisha sheria ya utumishi wa umma na Tume  ya Usuluhishi na Uamuzi  (CMA) akisema wajibu wa Serikali ni kutengeneza mazingira wezeshi kwa wafanyakazi na ipo tayari kupokea maoni katika kuongeza uzalishaji kupitia uwekezaji.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali  na Afya TUGHE, Archie Mntambo alileeza kwamba hivi sasa Chama hicho kina makakati wa kuboresha utendaji wake  kuendana na teknolojia iliopo sasa pamoja na kutenga bajeti ya kuwezesha uwepo wa mfumo huku akisisitiza wanachama kuendeleza amani  iliyopo ndani ya chama na demokrasia.

“Tunategemea kuwa na vitega uchumi yakiwemo majengo kuanzia Dodoma na tunatarajia kuwa na kamati ya maadili ya viongozi  na wanachama  pia kusimamia  masuala ya rushwa tuwe na TUGHE safi na imara tunaahidi kuendeleeza amani iliyojengeka  kwa thamani kubwa,”alifafanua Mwenyekiti huyo.

Katika hatua nyingine alikipongeza Chama hicho kwa kushiriki vyema katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Homa kali ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona akibainisha kwamba ni ugonjwa ulioikumba Dunia hivyo inahitajika nguvu ya pamoja kukabili maradhi hayo.

Kwa upande wake Msajili wa Vyama vya Wafanyakazi na Waajiri nchini Bi.Pendo Berege alipongeza Chama cha TUGHE kwa kuheshimu Katiba  na kuamua kufanya uchaguzi huo muhimu unaobeba mustakabali wa chama na Taifa kwa ujumla  akiwasihi wajumbe kuchagua viongozi bora.

Mbali na hayo  rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania  (TUCTA),Tumaini Nyamhokya aliwahimiza wanachama na viongozi wa TUGHE kuepuka mipasuko ndani ya Chama inayosababisha kudorora kwa utendaji kazi hivyo kutumia muda mwingi kutatua migogoro badala ya  kutimiza majukumu yao.

Aidha Katibu Mkuu Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGHE) Bwa.  Hery Mkunda alisema Chama hicho   kitaendelea kumuunga mkono Rais wa Awamu ya Sita Mhe. Samia Suluhu Hassan kuwaletea wananchi maendeleo na Chama kutumika kama nyenzo ya hamasa kwa wafanyakazi kujituma na kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria.




from MPEKUZI

Comments