Mahakama kutoa uamuzi kesi ndogo ya Freeman Mbowe na Wenzake Oktoba 19


Upande wa utetezi katika kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi, inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe na wenzake watatu, wamefunga ushahidi wao.

Ni baada ya mashahidi watatu kutoa ushahidi wa maelezo ya onyo ya mshtakiwa Adam Kasekwa aliyoyatoa Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam, ambayo upande wa utetezi walipinga maelezo hayo yasipokelewe makamani hapo kama kielelezo kwa madai yalichukuliwa nje ya muda kisheria, huku mshtakiwa huyo akidai  aliteswa wakati wa kuchukuliwa maelezo hayo.

Wakili wa utetezi, John Mallya ameieleza Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, leo Septemba 29, 2021 muda mfupi baada ya shahidi wa tatu katika kesi hiyo Liliani Kibona, kumaliza kutoa ushahidi wake.

Mbali na kufunga ushahidi huo, Mallya ameiomba Mahakama kuwasilisha majumuishi ya hoja kwa njia ya maandishi siku ya Jumatatu, Oktoba 4, 2021.

Ombi hilo limeungwa mkono na upande wa mashtaka, ambao na wao watawasilisha hoja zao kwa njia ya maandishi.

Baada ya kusikiliza maelezo hayo Jaji Mustapha Siyani amekubaliana na maombi hayo na kisha kuahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 19, 2021 kwa ajili ya uamuzi katika kesi hiyo ndogo na kisha upande wa mashtaka kuendelea na kesi ya msingi.

Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 16/2021 ni Halfan Mbwire Hassan, Adam Hassan Kasekwa na Mohamed Ling'wenya.


from MPEKUZI

Comments