Majaliwa: Sh. Bililioni 172 Zimetumika Kulipa Madeni Ya Watumishi


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema katika kipindi cha Mei 2021 hadi sasa Serikali imetumia sh. bilioni 172.614 kulipa madeni mbalimbali ya watumishi wa umma na inaendelea kulifanyia kazi suala hilo ili lisiendelee kuwa kero kwa wastaafu katika kumudu maisha baada ya kustaafu.

Pia, Waziri Mkuu ameuagiza uongozi wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Tanzania (TALGWU) uhakikishe unatumia fedha na rasilimali za chama hicho kwa kuwahudumia wanachama wao wote bila ubadhirifu.

Ametoa kauli hizo leo (Jumatano, Agosti 25, 2021) alipofungua mkutano TALGWU uliofanyika katika ukumbi wa Royal Village hotel jijini Dodoma.

“Hivyo, ninawaagiza waajiri wote wazingatie kanuni za kudumu katika Utumishi wa Umma za mwaka 2009 ili kuondoa changamoto ya watumishi kutolipwa gharama za kurejeshwa nyumbani na stahili zao nyingine mara baada ya kustaafu.”

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa wanaTALGWU na kuwasihi waendelee kushirikiana, kushikamana na kuwajibika kwa kuzingatia uadilifu kwani kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi ni silaha kuu katika kufikia malengo ili kupunguza mzigo kwa Serikali.

“Ninawahakikishia kwamba, wakati wote Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa vyama vya wafanyakazi katika kushughulikia maslahi kwa watumishi. Vilevile, hakikisheni fedha na rasilimali za chama zinatumika katika kuwahudumia wanachama wenu bila ubadhirifu..”

Kadhalika, Waziri Mkuu ametoa rai kwa viongozi watakao fanikiwa kuibuka kidedea katika uchaguzi watakaoufanya leo wahakikishe wanaenda kutekeleza majukumu yao ya kikatiba kwa weledi mkubwa na kwa kuweka maslahi ya wanachama wao mbele.

“Aidha, natambua kuwa harakati za uchaguzi zinapitia mchakato mkubwa wenye mambo mengi. Hata hivyo, nawasihi baada ya uchaguzi huu mkaimarishe umoja na mshikamano kwani hizo ndizo silaha kuu za kutetea haki na kuimarisha maslahi ya wafanyakazi nchini.”

Amesema hadi sasa zipo halmashauri 18 ambazo hazijaunda mabaraza ya wafanyakazi, hivyo amemuelekeza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Jenista Mhagama kuwaagiza Makatibu Wakuu wa Wizara husika wahakikishe mabaraza hayo yanaundwa ifikapo ama kabla ya tarehe 30 Septemba 2021.

Akizungumzia kuhusu ugonjwa wa UVIKO 19, Waziri Mkuu amewataka wananchi wafuate maelekezo yanayotolewa na wataalamu wa afya katika kujinga na ugonjwa huo na pale wanapoona dalili ambazo hawazielewi wawahi katika vituo vya kutolea huduma za afya kwa uchunguzi na matibabu.

 “Kama mnavyofahamu, kuwa dunia nzima ipo kwenye wimbi la tatu la UVIKO 19. Janga hili lipo nchini na limesababisha baadhi ya ndugu zetu kupoteza maisha na wengine kuendelea kuugua. Kwa msingi huo ni muhimu kwetu kuendelea kuchukua tahadhari kwa kujikinga na maambukizi ya UVIKO 19.”

Amesema kuwa chanjo ya UVIKO 19 inapatikana na inasambazwa nchini kote ikiwemo hapa Dodoma ambapo huduma hiyo inatolewa katika vituo 89 ndani ya mkoa. “Sambamba na vituo hivi, pia ipo huduma ya mkoba (mobile) ambapo watumishi wa afya wanakwenda katika maeneo yenye watu wengi ikiwemo makampuni ya ujenzi na kutoa huduma”

“Niwatoe hofu wananchi wote kuwa chanjo hii ni salama, haina madhara yoyote na ni hiyari na hakuna atakayechanjwa pasipo ridhaa yake. Hivyo, niwaombe wananchi kujiepusha na watu wanaopotosha ukweli kuhusu suala la chanjo.”

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Jenista Mhagama ametumia fursa hiyo kumpongeza Mhe. Rais Samia Suluhu Hassam na Waziri Mkuu kwa kusimamia vizuri vyama vya wafanyakazi ambavyo vinatetekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sheria, taratibu na miongozo.

Aidha, Waziri Mhagama amesema kuwa TALGWU  ni chama imara miongoni mwa vyama vya wafanyakazi nchini. “Sioni aibu kusema kwamba uongozi wa chama hiki cha TALGWU ni imara na unazingatia katiba,  kanuni na miongozo katika kuwatumikia wanachama wake.

Naye, Katibu Mkuu wa TALGWU, Rashidi Mtima amempongeza Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuchukua hatua madhubuti zenye lengo la kuondoa kero na kuimarisha maslahi ya wafanyakazi nchini.


from MPEKUZI

Comments