Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea kusimamia uhuru wa kuabudu kwa kila mwananchi kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Amesema kuwa Serikali itaendelea kuheshimu uhuru huo wa ibada zinazoendeshwa katika nyumba za dini na itaendelea kushirikiana na taasisi zote za dini na madhehebu yote kwa ajili ya ustawi wa taifa na watu wake.
Amesema hayo jana (Jumapili 29 Agosti 2021) Alipomuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan katika ibada ya kusimikwa kwa Askofu Mkuu wa Muungano wa Makanisa ya Umoja wa Pentekoste Tanzania Elieza Isaka Mazinge, katika kanisa la Pentekoste Wilaya ya Nzega Mkoani Tabora.
“Pale mtakapo pata tatizo lolote linalohitaji kutatuliwa na Serikali waoneni viongozi wa Serikali walioko katika maeneo yenu, Maelekezo ya serikali ni lazima viongozi hao waunge mkono jitihada za dini katika kufanya taifa hili kuwa tulivu.”
Akizungumza na waumini wa kanisa hilo, Waziri Mkuu amesema ni muhimu Watanzania kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kujiongezea kipato, kujiletea maendeleo ya mtu mmoja moja na Taifa kwa ujumla.
Amesema kuwa, Kwa sasa Nchi ya Tanzania iko katika uchumi wa kati na mafanikio hayo yametokana na kujitoa na kuchapa kazi kwa Watanzania na kuwataka kuendelea kudumisha amani na kuiunga mkono Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
“Nitoe rai kwa Watanzania kutokubwetekana na mafanikio yanayopatikana Nchini, endeleeni kufanya kazi kwa bidii katika sekta zote na malengo yetu ni kila Mtanzania ajipatie kipato halali, kulipa kodi na kuchangia ukuaji wa uchumi wa Nchi yetu.”
Aidha, Ametoa rai kwa Watanzania wanaoishi katika maeneo yanayoanza kupata Mvua za vuli na masika kutumia vyema fursa ya msimu wa mvua hizo kujishughulisha katika kilimo ili kupata mavuno mengi zaidi.
“Mavuno mengi yatatuhakikishia usalama wa chakula na kutupatia ziada ya kuuza ndani na nje ya nchi yetu na kwakufanya hivyo tutakuwa tumetekeleza maagizo ya maandiko matakatifu na ya Serikali
Waziri Mkuu amesema Serikali inatambua na kuunga mkono kamati za maendeleo ya kijamii zinazoundwa na viongozi wa dini na kuwasihi kutumia kamati hizo kuliombea Taifa na viongozi pamoja na kusimamia malezi ya vijana kuanzia ngazi ya familia kwa kutoa elimu ya kiroho.
Awali akisoma taarifa ya Kanisa hilo, Askofu Mkuu wa Muungano wa Makanisa ya Pentokoste Tanzania, Elieza Isaka Mazinge amesema kanisa linatambua jitihada za Serikali katika kupambana na janga la Uviko 19 hivyo kanisa limechangia mitungi ya oksijeni yenye thamani ya Shilingi Milioni mbili katika Hospitali ya Wilaya ya Nzega kwa ajili ya wagonjwa wenye changamoto ya upumuaji.
(Mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment