Hukumu Kesi ya Ole Sabaya na Wenzake Kutolewa October 01

Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, imepanga tarehe 1 Oktoba 2021, kutoa hukumu ya kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha, inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya na wenzake wawili.

Tarehe hiyo imepangwa leo Jumanne, tarehe 24 Agosti 2021 na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Odira Amworo, baada ya mahakama hiyo kumaliza kusikiliza ushahidi.


Katika kesi hiyo, washtakiwa wengine ni Sylvester Nyegu na Daniel Mbura.

Shahidi wa mwisho upande wa utetezi, ambaye alitoa ushahidi wake leo, alikuwa ni Mbura, akiongozwa na jopo la mawakili wa utetezi, likiongozwa na Wakili Dancan Oola.

Baada ya ushahidi huo kufungwa, Wakili wa Serikali Mkuu, Tumaini Kweka, aliiomba mahakama hiyo itoe siku saba kwa pande zote mbili, kuwasilisha majumuisho ya kesi hiyo kwa njia ya maandishi.

Hakimu Amworo alikubali ombi hilo na kutoa siku saba kwa pande zote mbili, kuwasilisha majumuisho hayo.

Katika Kesi hiyo, Sabaya na wenzake wawili wanaotuhumiwa Kwa makosa matatu ya unyang'anyi wa kutumia silaha katika duka la Mohamed Saad lililopo eneo la bondeni jijini Arusha Februari 9 mwaka huu.



from MPEKUZI

Comments