Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango, leo Julai 23, 2021 anatarajiwa kuanza ziara ya kikazi ya siku tano mkoani Mtwara.
Makamu wa Rais akiwa mkoani Mtwara anatarajiwa kushiriki misa ya kumbukizi ya mwaka mmoja wa kifo cha hayati Rais wa awamu ya tatu Benjamin William Mkapa katika Kijiji cha Lupaso Wilaya ya Masasi.
Aidha Makamu wa Rais anatarajiwa kuzindua stendi ya mabasi Wilaya ya Nanyumbu, soko la kisasa la matunda na mbogamboga la Jidah wilayani Masasi, kuzindua kiwanda cha kubangua korosho Wilaya ya Newala pamoja na kuzungumza na wananchi katika maeneo mbalimbali atakayotembelea.
Katika hatua nyingine Makamu wa Rais anatarajiwa kuweka jiwe la msingi Hospitali ya Kanda ya kusini iliopo Wilaya ya Mtwara na baadaye kuzungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara utakaofanyika katika viwanja vya sabasaba Mtwara mjini.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment