Waziri Mkuu Awataka Viongozi Waendelee Kusimamia Amani


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amefungua mafunzo ya Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa mikoa na kuwataka viongozi hao waendelee kusimamia amani na utulivu kwenye mikoa yao ili watu waendelee kufanya shughuli zao bila wasiwasi wowote.

“Amani na utulivu ndiyo itatuwezesha kama nchi, tuendelee kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuwekeza mitaji yao hapa nchini. Tunakumbushwa sisi viongozi wa Tanzania tuwe wazalendo na tuhakikishe tunaziendeleza rasilimali za nchi hii kwa faida ya Watanzania wote.”

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumatano, Juni 30, 2021) wakati akifungua mafunzo ya siku nne yaliyoandaliwa na Taasisi ya Uongozi kwa lengo la kuwaimarisha viongozi ili matokeo ya uongozi wao yawapatie majawabu endelevu wananchi dhidi ya changamoto mbalimbali zinazowakabili kwenye maeneo yao.  Mafunzo hayo yanafanyika jijini Dodoma.

Amesema baada ya mafunzo hayo Serikali inatarajia viongozi hao watasimamia kikamilifu nidhamu katika utumishi wa umma na kuwa kioo katika kuzingatia maadili na miiko bila kubagua jinsia, kabila, dini, rangi ya ngozi, mtu atokako ndani ya nchi ilimradi hajavunja sheria.

Waziri Mkuu ameongeza kuwa mafunzo yatawawezesha viongozi hao kusimamia kikamilifu miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika ofisi zao za mikoa na za Mamlaka za Serikali za Mitaa katika maeneo yao ya utawala na kuongeza udhibiti katika ukusanyaji na matumizi ya mapato ya ndani ya halmashauri.

“Mtazingatia kikamilifu mipaka yenu ya madaraka na hatua mtakazozichukua zitazingatia sheria, kanuni na taratibu zilizopo. Mtasimamia kikamilifu mapambano dhidi ya dawa za kulevya pamoja na kudumisha uhusiano baina yenu na watumishi walio chini yenu, kwa kuzingatia kuwa kila mtumishi anao mchango katika kuboresha utendaji kwenye kituo chake cha kazi.”

Waziri Mkuu amesisitiza viongozi hao kwamba lazima wawe makini muda wote na watumishi wazembe, wezi na wabadhirifu kwenye halmashauri zao lazima wote wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za Serikali. Ameagiza ubadhirifu ushughulikiwe mapema kwa weledi na utaalam bila kulazimika kusimamisha utekelezaji wa miradi kwa muda mrefu.

 “Lazima watu wachache ambao wamezoea kupanga njama za kijinai kuiba au kutumia vibaya fedha za umma washughulikiwe kisheria kama upo ushahidi wa wazi kabla hata CAG hajakagua au viongozi wa juu wachukue hatua wakati ninyi mpo. Lazima mianya yote ya ubadhirifu izibwe na tusioneane haya.”

Pia, Waziri Mkuu ametoa wito kwa viongozi hao kuwa wa wakafanyeni kazi kwa uadilifu kulingana na viapo vyao na kila mmoja katika eneo lake awe msimamizi mzuri na kutanguliza mbele maslahi mapana ya Taifa, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati.

Akizungumzia kuhusu miradi ya maendeleo kutokamilika kwa wakati na kwa ukamilifu, Waziri Mkuu amesema kuna changamoto ya baadhi ya miradi katika kutokukamilika kwa wakati na kwa kiwango kilichokusudiwa. “Pamoja na sababu nyingine tumebaini pia kuna baadhi ya viongozi huingilia michakato ya zabuni, manunuzi na ya ujenzi ikiwa ni katika hatua mbalimbali na wengine wanakwenda mbali zaidi kudai wapewe asilimia 10 ya fedha.”

“Nieleze bayana kuwa hili sasa tunalifuatilia kwa karibu na hatutakuwa na uvumilivu pale tutakapowabaini.  Nisistize kuwa Serikali ina macho mengi tutakapopata taarifa za baadhi yenu kujihusisha na vitendo vya ubadhirifu wa fedha za Serikali kupitia fedha zinazoletwa za Miradi ya Maendeleo au zile zinazokusanywa na Halmashauri hatua kali zitachukuliwa dhidi yenu.”

Mafunzo hayo yamehudhuriwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Ummy Mwalimu, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mohamed Mchengerwa, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, David Silinde, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Festo Dugange.

Wengine ni Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Prof. Riziki Shemdoe, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Laurean Ndumbaro, Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais - TAMISEMI; (Elimu), Gerald G. Mweli, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais – TAMISEMI (Afya), Dkt. Grace E. Magembe  na Afisa Mtendaji Mkuu, Taasisi ya Uongozi, Kadari Singo.

(Mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU


from MPEKUZI

Comments