Kauli ya Rais Samia juu Katiba Mpya na mikutano ya hadhara


Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amewataka Watanzania kumpa muda aimarishe uchumi wa nchi ili aweze kuangalia suala la Katiba Mpya na mikutano ya hadhara ambayo kwa sasa imezuiwa.

Ameeleza hayo  jana Jumatatu Juni 28, 2021 wakati akijibu maswali mbalimbali ya wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini aliokutana nao Ikulu jijini Dar es Salaam,  yakiwemo ya mchakato wa Katiba Mpya na kuzuiwa kwa mikutano hiyo.

“Kama inavyosemwa nimeanza vizuri naomba nipeni muda nisimamishe nchi kwanza kiuchumi. Tuite wawekezaji wawekeze ajira zipatikane uchumi ufunguke halafu tutashughulikia Katiba, tutashughulikia mikutano ya hadhara wakati ukifika.

“Kwa sasa tunaruhusu mikutano ya ndani ya vyama  na wabunge wapo huru kufanya mikutano ya hadhara katika maeneo yao si maeneo ya wengine..., ile yeyeee ingieni..., hili naomba sana Watanzania tujipe muda tufanye uchumi wetu..., sisemi katiba si ya maana lakini naomba mnipe muda kwanza nisimamishe uchumi kisha tutatizama mengine,” alisema Samia.

Alisema katika hotuba yake bungeni hivi karibuni alieleza atakutana na viongozi wa vyama vya siasa ili kujadili mustakabali wa siasa na Taifa.

“Sasa hivi nchi yetu ina changamoto nyingi sana, kuna janga la corona, uchumi umeshuka tunatakiwa kuupandisha. Na hili nataka niliunganishe na lile la Katiba Mpya. Kuna mambo mengi ya kushughulikia, nimesema ninakwenda kuifungua nchi kwa sababu uchumi umeshuka tunatakiwa kupandisha uchumi, tukifungua nchi.”

“Kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji kazi ambayo tumeifanya vizuri sana nataka niwaambie wawekezaji waliosajiliwa kipindi cha Machi hadi Mei mwaka huu ni mara mbili ya waliosajiliwa mwaka jana kipindi kama hiki,” alisema Samia.



from MPEKUZI

Comments