Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Pauline Gekul ameiagiza Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo kuanzisha utaratibu wa mafunzo kwa kutumia mitandao ili kuwafikia vijana wengi Mikoani ambayo yatasaidia katika kukuza vipaji vya vijana hao.
Naibu Waziri Gekul ameyasema hayo Mei 22, 2021 Wilayani Bagamoyo alipotembelea Taasisi hiyo ambapo amesema uhitaji wa mafunzo ya kukuza vipaji ni mkubwa kwa maeneo mbalimbali nchini lakini vijana wengi wanashindwa kufika katika Taasisi hiyo kutokana na changamoto ya ukosefu wa fedha.
“Vijana wanahitaji haya mafunzo ila kuna changamoto ya uhaba wa majengo ya mabweni pamoja na gharama za mafunzo, TaSUBa mkienda Mikoani na kutumia njia ya mitandao mtakuwa mmewafikia vijana ambao kupitia vipaji vyao watajiajiri na kujipatia vipato "amesema Mhe. Gekul.
Kwa upande wake Mkuu wa Taasisi hiyo, Dkt. Herbert Makoye amesema Taasisi hiyo imeanza kutekeleza suala hilo na tayari muitikio ni mkubwa kwa maeneo waliyofika na wataendelea kutekeleza maagizo hayo.
Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo ni moja ya Taasisi kongwe nchini zinazotoa mafunzo yanayosaidia kunoa vipaji mbalimbali vinavyotokana na Sekta za Sanaa pamoja na Utamaduni ambazo zinachangia kutoa ajira pamoja na kuchangia pato la Taifa.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment