Waziri wa Afya Dkt. Dorothy Gwajima Akutana Na Balozi Wa China Mhe. Wang Ke


Na.WAMJW-Dodoma
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima leo tarehe 29 Aprili 2021 amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa China nchini Tanzania Mhe. Wang Ke katika ofisi za Wizara jijini Dodoma.

Pamoja na mambo mengine Balozi Wang amemueleza Waziri Gwajima kuwa Serikali ya China itaendeleza ushirikiano uliopo baina ya nchi hizo katika suala la kuleta wataalam mbalimbali wa Afya nchini.

Balozi huyo amesema Serikali ya China iko tayari kushirikiana na Tanzania kwa kutoa uzoefu wa namna walivyokabiliana na janga la Corona ili kuwawezesha wananchi kuendelea na shughuli za kibishara na uzalishaji ili kukuza uchumi katika nchi zote mbili.

Aidha, Mazungumzo hayo yalijikita pia katika kuunda timu ya pamoja ya wataalam itakayokua ikichambua maeneo ya ushirikiano na kuwasilisha katika uongozi wa juu wa nchi zote ili kufanya maamuzi.

Vilevile Serikali ya China imetoa mkopo kwa ajili ya upanuzi wa majengo ya Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), lengo likiwa kuiwezesha taasisi hiyo kutoa huduma za kibingwa na bobezi za Moyo.

Kwa upande mwingine, Waziri Gwajima na Balozi Wang walizungumzia kuendeleza ushirikiano baina ya nchi hizo mbili yaliyoasisiwa na viongozi wa nchi hizo toka miaka 1960.


from MPEKUZI

Comments