Angela Msimbira TAMISEMI
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Ummy Mwalimu ameagiza Halmashauri ambazo zimekusanya mapato chini ya asilimia 75 ya makisio yake kufanya tathmini na kuhakikisha inaweka mikakati madhubuti ya kufikia malengo yao ifikapo 30 Juni, 2021.
Akitoa taarifa ya ukusanyaji wa mapato ya ndani ya Halmashauri kwa kipindi cha Julai, 2020 hadi machi, 2021 Waziri ummy amesema kila Halmashauri ihakikishe inatumia kwa usahihi mifumo ya kielektroniki ya ukusanyaji wa mapato ya ndani na mifumo ya uhasibu ili kutoa taarifa kwa kufuata matakwa kwa kuzingatia viwango vya kimataifa vya uhasibu katika sekta ya umma (IPSAS).
Waziri Ummy ameiagiza Mikoa kuendelea kusimamia, kutoa ushauri na maelekezo kuhusu suala zima la ukusanyaji na matumizi ya mapato ya ndani ya Halmashauri kabla ya viongozi wa juu kubaini matatizo ya halmashauri nchini.
Amezielekeza Halmashauri zote nchini kuzuia na kudhibiti matumizi ya fedha mbichi kabla ya makusanyo hayajapelekwa benki, kwa kuwa kwa mujibu wa sheria fedha inatakiwa kukusanywa na kupelekwa benki ndipo kuanza kutumika.
Waziri Ummy amewaagiza wakurugenzi wa Halmashauri kuacha kutumia fedha mbichi za makusanyo kabla ya kupelekwa benki na atakayekiuka hatua kali zitachukuliwa dhidi yake kwa kuwa atakuwa amekiunka miongozo ya kifedha inayomtaka kuhakikisha wanankusanya na kupeleka benki ndipo kuanza kutumika.
Ameielekeza Mikoa kuendelea kusimamia Halmashauri kwa kutoa taarifa kupitia mifumo ya kielektroniki, kusisitiza usuluhishi wa taarifa na usahihishaji wa takwimu katika mifumo mbalimbali na kuongeza jitihada katika usimamizi wa ukusanyaji wa mapato ya ndani katika Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Hata hivyo, amezitaka Sekretarieti za Mikoa kuhakikisha wanatoa ushauri stahiki kwa wakati, kutatua changamoto zilizopo katika suala zima la ukusanyaji wa mapato katika halmashauri wanazoziongoza, kutoa miongozo kwa lengo za kuhakikisha Mamlaka za Serikali za Mitaa zinafanya vizuri katika suala zima la ukusanyaji wa mapato ili kuleta maendeleo kwa wananchi
Akizungumzia ukusanyaji wa Mapato hayo Waziri Ummy ameeleza kwa mwaka wa fedha 2020/21 Halmashauri zilipanga kukusanya Shilingi Bilioni 814.96 kutoka kwenye vyanzo vyake vya ndani katika kipindi cha Julai, 2020 hadi Machi, 2021 Halmashauri zimeweza kukusanya jumla ya shilingi bilioni 557.45 sawa na asilimia 68 ys makisio ya mwaka
Amefafanua kuwa taarifa za mapato ya vyanzo vya ndani vya Halmashauri katika kipindi cha Julai 2020 hadi Machi, 2021 imeonesha uwepo wa ongezeko la mapato yaliyokusanywa kuwa ni shilingi bilioni 30.14 ikilinganishwa na kiasi kilichokusanywa katika kipindi kama hicho cha Julai – Machi , 2020 sawa na ongezeko la asilimia 6.
Waziri Ummy ameongeza kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Msalala imeongoza kwa kukusanya mapato kwa asilimia 117 ya makisio yake ya mwaka wakati Halmashauri za Wilaya za Ngorongoro imekuwa ya mwisho kwa kukusanya chini ya asilimia 34 ya makisio yake ya mwaka.
Katika kuzipima Halmashauri zote kwa kigezo cha wingi wa mapato (pato ghafi), Halmashauri ya Jiji la Dar-es-salaam imekusanya mapato mengi zaidi kuliko Halmashauri zote kwa kukusanya shilingi bilioni 52.78 na Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe imekusanya mapato kidogo kuliko Halmashauri zote kwa kukusanya Shilingi Milioni 453.72
Hata hivyo katika ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri Kimkoa kwa kuzingatia asilimia ya makusanyo Waziri Ummy amebainisha kuwa Mkoa wa Geita umefanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato ya ndani ambapo umekusanya kwa wastani wa asilimia 82 ya makisio ya mwaka ya Halmashauri za Mkoa huo wakati Mkoa wa mwisho kwa kigezo hicho ni Mkoa wa Singida ambao umekusanya wastani wa asilimia 48 ya makisio ya mwaka ya Halmashauri za Mkoa huo.
Katika hatua nyingine Waziri Ummy ameweka wazi Ukusanyaji wa Mapato ya Ndani ya Halmashauri Kimkoa kwa Kuzingatia Wingi wa Mapato kuwa Mkoa wa Dar es Salaam umefanya vizuri kwa kigezo cha wingi wa mapato ambapo imekusanya kiasi cha Shilingi Bilioni 133.90 huku Mkoa wa mwisho katika wingi wa mapato ni Mkoa wa Rukwa ambao umekusanya Shilingi Bilioni 5.57.
Vile vile Ukusanyaji wa mapato kwa Halmashauri kwa Kuzingatia aina ya Halmashauri kwa Kigezo cha asilimia ya makusanyo ukilinganisha na makisio ya mwaka Waziri Ummy amesema kwa upande wa Majiji Halmashauri ya Dar-es-salaam imeongoza kwa kukusanya mapato kwa asilimia 78 ya makisio yake ya mwaka na Halmashauri ya Jiji la Dodoma imekuwa ya mwisho katika kundi hili ambapo imekusanya kwa asilimia 58 ya makisio yake ya mwaka.
Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni imeongoza kundi la Halmashauri za Manispaa ambayo imekusanya asilimia 101 ya makisio yake na Katika kundi hilo Halmashauri ya Manispaa ya Lindi imekuwa ya mwisho ambapo imekusanya kwa asilimia 36 ya makisio yake ya mwaka.
“Kwa kundi la Halmashauri za Miji , Halmashauri ya Mji Kibaha imeongoza kwa kukusanya kwa asilimia 93 ya makisio ya mapato ya ndani kwa mwaka wa fedha 2020/21 ambapo Halmashauri ya Mji wa Bariadi imekuwa ya mwisho kwa kukusanya asilimia 36 ya makisio ya mapato ya ndani kwa mwaka wa fedha 2020/21” amesema Waziri Ummy
Aidha, kwa upande wa Halmashauri za Wilaya amesema Halmashauri ya Wilaya ya Msalala imeongoza kwa kukusanya asilimia 117 ya makisio ya mapato ya ndani huku Halmashauri za Wilaya za Ngorongoro kuwa ya mwisho katika kundi hilo kwa kukusanya asilimia 34 ya makisio ya mapato ya ndani kwa mwaka wa Fedha 2020/21.
“Halmashauri ya Jiji la Dar-es-salaam a imeongoza kwa kundi la Halmashauri za Majiji kwa kigezo cha wingi wa mapato kwa kukusanya Shilingi bilioni 52.78 na Halmashauri ya Jiji la Tanga imekuwa ya mwisho katika kundi hili ambapo imekusanya Shilingi bilioni 9.93.” ameeleza Waziri Ummy
Kwa kuongezea Waziri Ummy amesema kwa upande wa Halmashauri za Manispaa,Manispaa ya Kinondoni imeongoza kwa kukusanya Shilingi bilioni 33.25 na Halmashauri ya Manispaa ya Lindi imekuwa ya mwisho katika kundi hili ambapo imekusanya Shilingi bilioni 1. 26
Huku katika kundi la Halmashauri ya Wilaya, Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze imeongoza kwa kukusanya mapato mengi ambapo imekusanya Shilingi Bilioni 6.48. Aidha, Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe imekuwa ya mwisho katika kundi hili ambapo imekusanya Shilingi Milioni 453.72
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment