Makampuni 49 ya Kitanzania yameidhinishwa na Mamlaka ya Forodha Nchini China ili kuuza Maharage ya Soya (Soya Beans) kutoka Tanzania kwenda Nchini China.
Taarifa iliyotolewa na Mhe. Mbelwa Kairuki, Balozi wa Tanzania Nchini China alipofanya mawasiliano na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) kwa njia ya mtandao imesema kuwa mafanikio ya hatua hizi ni matokeo ya mkataba uliosainiwa baina ya nchi ya Tanzania na China mwezi Oktoba, 2020 ambapo Nchi ya China iliruhusu Nchi ya Tanzania kusafirisha bidhaa hiyo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) Bw. Edwin Rutageruka amesema kuwa haya ni mafanikio ya kazi kubwa inayoendelea kufanywa na TanTrade ya kuunganisha wafanyabiashara wa hapa nyumbani Tanzania na wa nchi mbalimbali ambazo Balozi zetu zinatuwakilisha “tumekuwa na Mikutano ya kibiashara kwa njia ya mtandao tokea mwezi wa Julai, mwaka 2020 ya kuwaunganisha Wafanyabiashara wa Nchi za Mashariki ya Kati na Asia ikiwemo Malaysia, Indonesia na Ufilipino pamoja na Nchi za Arabuni zikiwemo Saudi Arabia, Kuwait, Qatar na Oman kwa kushirikiana na Mabalozi wetu katika nchi hizo na hatimae mikutano hiyo imeonesha mafanikio” alisema Bw. Rutageruka.
Aliongeza kuwa, China ni soko kubwa na uhitaji wao ni tani milioni 103 kati ya tani milioni 88 zinaagizwa kutoka mataifa mbalimbali na tayari Tanzania imefanikiwa kusafirisha tani 142 za Maharage ya Soya tarehe12 Machi, 2021 Nchini China na inatarajia kusafirisha zaidi ya tani 13,000.
Rutageruka ametoa wito kwa wakulima wa Tanzania waitumie Wizara ya Kilimo kuwasaidia katika uwezo wa kuzalisha maharage ya aina ya soya ili wakidhi viwango vinavyohitajika na soko hilo la China.
Pia amewapongeza Watanzania wanaochangamkia fursa zinazotangazwa na Serikali, ambapo amesema kazi ya Serikali ni kuonesha fursa za masoko pamoja na kutengeneza mazingira ya ufanyaji biashara kama kuingia makubaliano na nchi mbalimbali ili wafanyabiashara wa Tanzania waweze kupenya katika masoko mbalimbali ambapo kazi hii imeshafanyika kupitia ubalozi wetu wa Tanzania uliopo Beijing China.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment