Waziri Mhagama atoa utaratibu wa mazishi ya Dkt. Magufuli

 Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, amesema ratiba ya misa takatifu ya mazishi ya Dkt. John Magufuli itaanza saa 12:30 alfajiri ambapo wananchi wataanza kuingia katika Uwanja wa Magufuli wilayani Chato.

Waziri Mhagama amezungumza hayo baada ya kumalizika kwa zoezi la kuaga mwili wa Dkt. Magufuli kwa wakazi wa Geita na maeneo jirani. Amewataka wananchi kuwahi ili taratibu nyingine ziweze kuendelea.

Amesema majira ya saa 1:30 asubuhi viongozi mbalimbali wataanza kuwasili katika uwanja huo kwa ajili ya kumsubiri Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

Ameeleza kuwa kabla ya mwili kuletwa uwanjani, itafanyika misa fupi nyumbani kwa marehemu ambayo itahusisha wanafamilia, ikiwa ni misa yao ya mwisho na mwili wa mpendwa wao kabla haujazikwa katika eneo hilo la nyumbani.

Mwili unatarajiwa kupolelewa Uwanja wa Magufuli majira ya saa 3:00 asubuhi tayari kwa misa takatifu ambayo amedokeza kuwa kati ya maaskofu watano hadi 10 wataongoza misa hiyo.

Viongozi mbalimbali watapata nafasi ya kutoa salamu fupi ambazo zitahitimishwa na Rais Samia Suluhu Hassan, kabla ya mwili huo kurudishwa nyumbani kwa ajili ya kuwekwa katika nyumba yake ya milele.

Amesema aneo la nyumbani atakapozikwa Dkt. Magufuli ni dogo hivyo si watu wote watakaoweza kufika hapo, hivyo amewaomba wale watakaoshindwa, kuridhia hali hiyo.

Dkt. Magufuli alifariki Dunia Machi 17, 2021 katika Hospitali ya Mzena Dar es Salaam kwa maradhi ya moyo.



from MPEKUZI

Comments